Mwanza. Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Seke Mabirika (45) kwa tuhuma ya mauaji ya mke wake, Rahel Mabina (39) kwa kumshambulia kwa ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake.
Tukio hilo limetokea jana Alhamisi Januari 15, 2026 saa 1:00 asubuhi, katika Kitongoji cha Tinda, kata ya Mwamabanza wilayani Magu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo imetolewa leo Ijumaa Januari 16, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, mtuhumiwa huyo anadaiwa kumshambulia mke wake aliyekuwa na ujauzito wa miezi miwili tumboni na sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kupoteza nguvu na hatimaye kufariki dunia.
Mutafungwa amesema chanzo cha mauaji hayo ni kutokana mgogoro wa kifamilia uliozuka baina ya mtuhumiwa na marehemu ambaye alidai fedha za matumizi.
“Taarifa kuhusiana na chanzo cha mauaji haya ni mgogoro wa kifamilia uliotokana na marehemu kudai fedha ya matumizi kwa mume wake, na inaonekana kuwa marehemu alikuwa mke wa tatu wa mtuhumiwa na wamebahatika kupata mtoto mmoja,” amesema Mutafungwa.
Amesema mwili wa marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa uchunguzi wa kitaalamu huku mtuhumiwa akiendelea kuhojiwa na upelelezi utakapo kamilika atafikishwa mahakamani kwa taratibu za kisheria.
Kamanda huyo, amewataka wananchi kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia badala yake wakumbuke kufanya mazungumzo yatakayoleta maelewano katika familia zao ili kuepuka matukio ya mauaji.