Pemba. Juma Suleiman Juma (51) mkazi wa Pujini Kibaridi Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, amefariki dunia baada ya kudondokewa na jiwe wakati akichimba mawe kwenye machimbo ya Makaani Pujini.
Wakizungumza na Mwananchi leo Januari 16, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo ambao ni miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho walioshiriki shughuli ya kuuopoa mwili, wameeleza namna walivyopata taarifa za tukio hilo na kuanza harakati za uokozi.
Ali Suleimana Juma ni kaka wa marehemu na mkazi wa Kijiji Cha Pujini amesema muda mfupi walikuwa pamoja kwenye eneo hilo ingawa yeye alirejea nyumbani, lakini baadaye alipata taarifa za ndugu yake kuangukiwa na kifusi.
Amesema alipofika kwenye eneo la tukio na kushirikiana na wahisani wengine walianza kuutafuta mwili, walifanya juhudi ya kulivunja jiwe hilo ili kumtoa marehemu lakini walishindwa.
Ridhiwani Asaa Abdalla mkazi wa Kibaridi Pujini amesema walipofika kwenye tukio waliona hali ni mbaya katika kuutafuta mwili wa marehemu huyo kutokana na kiambaza kizima cha jiwe kumuangukia.
Amesema walijitahidi kuvunja mawe juhudi hizo ziligonga mwamba na kuwasiliana na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kuja kushirikiana katika kuutafuta mwili wa kijana huyo.
”Kwa kweli nilipofika niliona hali ngumu jiwe kubwa lililomuangukia tukaanza kulikata lakini hata hivyo ilishindikana tukaamua kuwasiliana na wenzetu wa uokoaji kuja kusaidiana katika kuokoa mwili huo,” amesema.
Suleiman Hilali Abdalla amesema walivunja jiwe hilo na kuona mwili, lakini hawakufanikiwa kuupata ndipo ilipokuja skaveta kusaidia katika uokoaji.
Kamanda wa Operesheni wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Pemba, Mbarouk Ali Juma amesema wamepokea taarifa hizo na kufika eneo hilo kushirikiana na wananchi lakini kutokana na ukubwa wa jiwe walilazimika kuomba msaada kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya kupata skaveta.
”Tulipofika eneo ya tukio tuliwasiliana na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kutuletea Skaveta na walipokuja nalo tukaendelea naendelea na harakati za Uokozi tukafanikiwa kuupata mwili lakini kwa taarifa za daktari alikuwa alimeshafariki dunia,” amesema.
Akizungumza kufuatia tukio hilo Mkurugenzi wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame ametoa wito kwa wananchi hasa wanaofanya kazi ya uchimbaji wa mawe kufuata taratibu za kiusalama wakati wanapotekeleza majukumu yao.
”Niwaombe wananchi mchukue tahadhari wakati mnapofanya shughuli zenu hizi muangalie usalama wenu kwanza, tayari huyo alishapoteza maisha na sisi tuwe makani katika kufanya harakati zenu,” amefafanua.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo ametoa mkono wa pole kwa familia na marehemu huyo na kuwataka kuwa na subra katika kipindi hichi kigumu baada ya kuondokewa na Mwenza wao.
Tukio kama hilo lilitokea Juni 29/2025 katika Kijiji cha Mjini Wingwi Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo watu wawili wa familia moja walipoteza maisha.