Ashikiliwa kwa mauaji ya watoto watatu wa familia moja

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Dotto Lubogeja kwa tuhuma za kuwaua watoto watatu wa familia moja kwa kuwanyonga kisha kuiba ng’ombe 15.

Imeelezwa kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo baada ya kuwakuta watoto hao wakichunga ng’ombe katika eneo jirani na nyumba wanayoishi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa amesema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Ijumaa, Januari 16, 2026.

Siwa amesema tukio hilo lilitokea jana Januari 15, 2026 katika Kijiji cha Matundasi, Kata ya Matundasi, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya.

Amewataja watoto waliouawa kuwa ni Petro Amos (8), Sam Amos (6) na Nkamba Amos (4), wote wa familia moja na wakazi wa Kijiji cha Matundasi, Wilaya ya Chunya.

Amesema mtuhumiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo aliiba ng’ombe 15 waliokuwa wakichungwa na watoto hao.

“Baada ya kuiba ng’ombe, mtuhumiwa alienda kuwaficha nyumbani kwa mjomba wake, aliyetajwa kwa jina la Masoud Kurwa, mkazi wa Kijiji cha Matundasi (B), kisha kuanza kutafuta wateja,” amesema Siwa.

Amesema mtuhumiwa alifanikiwa kuuza mifugo hiyo kwa thamani ya Sh5.1 milioni.

Amesema kufuatia tukio hilo, polisi walianza msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa pamoja na mjomba wake aliyehusika kuficha ng’ombe hao.

“Katika msako huo, polisi walifanikiwa kupata ng’ombe 15 pamoja na fedha taslimu Sh5.1 milioni zilizopatikana baada ya kuwauza,” amesema.

Kaimu Kamanda huyo amesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha mauaji hayo ni tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali na kukatisha uhai wa watoto wasio na hatia.

Aidha, Siwa amewaonya wananchi kuacha tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo hivyo na litawachukulia wahusika hatua kali za kisheria.

Mkazi wa eneo hilo, Joyce Joel ameiomba Serikali na Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali dhidi ya mtuhumiwa huyo.

“Kimsingi inaumiza sana, kwani hawa walikuwa kizazi kijacho. Serikali ione namna ya kuweka sheria kali ili kutokomeza matukio ya aina hii,” amesema.