Dar es Salaam. Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imefuta uteuzi wa wenyeviti na makatibu wa kamati za kudumu za chama hicho, Kanda ya Nyasa.
Januari mosi, 2026 Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu alifanya uteuzi wa makatibu na wenyeviti wa kamati za kudumu wa kanda hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Sugu, viongozi walioteuliwa ni Fanuel Siame (mwenyekiti wa kamati ya fedha) na katibu wake ni Angumbwike Ntuli, kamati ya ilani itaongozwa na Leonard Fumbo na Elijah Simbeye (katibu).
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, kamati ya mafunzo itaongozwa na Frank Nkana (mwenyekiti) na Emily Mwakilembe (katibu), kamati ya wagombea, Obadia Mwaipalu (mwenyekiti) na Neema Kasinge (katibu), kamati ya ujenzi, Bruce Nyamwangi (mwenyekiti) na Frank Kifunda (katibu).
Wengine ni kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) mwenyekiti ni Daniel Naftari na Fikiri Zambi (katibu), kamati ya sheria na haki ya binadamu, mwenyekiti ni Fredrick Kihwelo na Irene Mhando (katibu) wakati kamati ya Chadema msingi itaongozwa na Pascal Haonga (mwenyekiti).
Hata hivyo, uteuzi huo, uliibua mvutano na kupingwa na baadhi ya wajumbe wa Kanda ya Nyasa walioandika barua ya malalamiko katika ofisi ya katibu mkuu wa Chadema, wakiitaka iingilie kati.
Miongoni mwa mambo waliokuwa wakilalamikia ni kutofuatwa kwa mchakato wa kamati utendaji kupokea mapendekezo ya sekretarieti na kuleta majina ya wajumbe na makatibu wa kamati.
Aidha, wajumbe hao waliupinga uteuzi huo wakidai haukufuata utaratibu, lakini katibu wa kanda hiyo, Grace Shio ameieleza Mwananchi mchakato huo ni utaratibu na miongozo ya chama hicho.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, ofisi ya katibu mkuu wa chama Januari 13, 2026 ilitoa maelekezo ya kufuta uteuzi huo na kutoa utaratibu upya wa kufuatwa.
Hata hivyo, Jumatano Januari 14, 2026 Mwananchi ilizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa lakini hakuweka wazi hatua walizozichukua katika sakata hilo, zaidi ya limefanyiwa kazi.
“Kikao kilikaa, lakini kuna mambo ambayo ya kiutawala zaidi, kuna barua zitakazowafikia wahusika kwa njia ya kiutawala siwezi kuweka kwenye magazeti.”
“Suala lao limefanyiwa kazi, kwa sababu ni jambo la kiofisi limefika. Yaliyobaki ni mambo ya kiutawala si mambo ya kutikisa, tumeshatoa maelekezo ya mambo ya kiutawala yanayopaswa,” amesema Golugwa.
Jana, Alhamisi Janauri 15, 2025 Mwananchi limemtafuta Shio kujua kama wamepata maelekezo, amejibu: “Sasa kama naibu amejibu kwa nini asikwambie? Hadi sasa mimi sijapata taarifa.”
Taarifa ambazo Mwananchi inazo zinadai barua ya maelekezo yenye kichwa ‘majibu ya malalamiko dhidi ya ubatili wa kikao cha kamati ya utendaji ya Kanda ya Nyasa imeamuru utaratibu huo uanze upya.
Inadaiwa suala la utaratibu kutofuatwa kwenye uteuzi wa wajumbe hao, ni miongoni mwa mambo yanayosababisha ofisi ya katibu mkuu wa chama hicho, kufuta mchakato huo na kuelekeza uanze upya.
Kilichobaki ni uongozi wa Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe na Rukwa kujipanga upya ili kuanza mchakato huo wa uteuzi wa wajumbe wapya wa kamati za kudumu.
Mmoja wa makada wa Chadema (jina tumelihifadhi), amesema majukumu ya kamati za kudumu za kanda yanategemeana na hazina tofauti na zile kamati za kiufundi.
“Mfano kamati ya fedha, kazi yake ni ‘kudeal’ na mambo ya fedha ikiwamo kufanya hamasa ya watu kutafuta fedha kwa ajili ya shughuli za chama. Pia, kazi yake nyingine kusimamia matumizi ya fedha.
“Ukienda kwenye kamati za Tehama au mafunzo ndio hivyo hivyo, zimepewa majukumu sawa sawa ya kiufundi. Kwa jumla kamati za kudumu zinaisaidia majukumu ya kamati ya utendaji ya kanda,” amesema kada huyo.
Kada huyo ametoa mfano kwenye suala la fedha, kamati hizo ndizo zenye jukumu la kuandaa ripoti au mpango utakaoidhinishwa na kamati ya utendaji ya kanda husika.
