HUENDA taarifa hii ikawapa ahueni mashabiki na wapenzi wa Simba, baada ya kuelezwa lile dili la kiungo mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua kutua Raja Casablanca huenda likafa kutokana na kocha Fadlu Davids kumnyakua kiungo mpya kutoka Ujerumani.
Ipo hivi. Fadlu aliyewahi kuinoa Simba na aliyehusika kumsajili Ahoua Msimbazi na kufanya naye kazi msimu uliopita timu hiyo ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, alikuwa akimpigia hesabu kiungo huyo raia wa Ivory Coast ili aungane naye pale Morocco.
Hata hivyo, kutokana na mambo kuwa mengi, kocha huyo Msauzi aliyerejea Raja Casablanca aliyekuwa akiinoa awali kama kocha msaidizi kabla ya kutua Msimbazi amekausha baada ya mabosi wa klabu hiyo ya Morocco kumnasa fundi mwingine aliyekuwa akitamba Ujerumani.
Fadlu na Raja wamefanya usajili wa kishindo kwa kumshusha kiungo huyo, Aymen Barkok aliyewahi kutamba na timu za Eintracht Frankfurt na Schalke 04 za Ujerumani.
Hatua ya Fadlu na klabu ya Raja kwa ujumla kumshusha kiungo huo inadaiwa inatokana na kupata ugumu wa kumnasa Ahoua waliyekuwa wakimpigia hesabu kumng’oa Msimbazi aliko kwa sasa.
Barkok, mwenye umri wa miaka 27, alizaliwa Frankfurt na alipitia akademi ya vijana ya Eintracht, akicheza mechi yake ya kwanza mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 18.
Alitwaa Kombe la DFB Pokal la Ujerumani msimu wa 2017/18 na pia alishinda Kombe la UEFA Europa League akiwa na Frankfurt mwaka 2022.
Kwa ujumla kiungo huyo amecheza mechi 113 za Bundesliga akichezea Frankfurt, Mainz 05 na Fortuna Düsseldorf, ingawa mkataba wake wa mwisho ulikuwa na Schalke 04 inayoshiriki Bundesliga 2.
Hata hivyo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Morocco sasa amekamilisha uhamisho wake kwenda Raja, ambapo atalenga kusaidia Fadlu na benchi lake la ufundi kuwania na hatimaye kutwaa taji la Botola Pro.
Kutokana na kutua kwa Barkok, huenda ikawa nafuu kwa Simba kusaliwa na Ahoua aliyemaliza kama kinara wa mabao wa klabu hiyo na Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga 16 na kuasisti tisa na kuifanya ahusike na mabao 25 akiiwezesha Sim,ba kumaliza nafasi ya pili na pia kutinga fainali ya CAF na kupoteza kwa mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco.
Msimu huu Ahoua ameshindwa kuonyesha makali akipoteza namba katika kikosi cha kwanza tangu alipoondoka kwa Fadlu, kiasi cxha kuibuka kwa tetesi kwamba alianzisha mgomo baridi wa kutaka kuachwa asepe na kuchelewa kambi ya timu hiyo iliyo chini ya kochga Steve Barker.
Hata hivyo, inaelezwa mabosi wa Simba wamechuna kumuachia nyota huyo kwa kumsikilizia kwanza kocha huyo mpya aliyetua kutoka Stellenbosch aliyemtumia katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 ambayo Simba ilipoteza mbele ya Azam FC kwa bao 1-0.
Licha ya kwamba dili la kwenda Raja linaelezwa limekufa, lakini nyota huyo inadaiwa anauzwa na Simba katika klabu nyingine iliyopo Uarabuni.
“Ahoua sidhani kama ataendelea kuitumikia Simba kwa mechi zilizosalia, kwani inaelezwa kuna klabu imemalizana na viongozi na wakati wowote ataondoka kwenda kujiunga,” kilisema chanzo hicho na kuutaka uongozi wa Simba utafutwe, ambapo hata hivyo hawakupatikana kwa njia ya simu.
