Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi amesema licha ya uwekezaji katika sekta ya uchukuzi kuhitaji gharama kubwa, Serikali imejipanga kikamilifu kuiboresha sekta ya anga kwa lengo la kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuimarisha mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Akizungumza leo Ijumaa, Januari 16, 2026, kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa jengo la kisasa la viongozi mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dk Nchimbi amesema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kupokea wageni wa hadhi ya urais watano kwa wakati mmoja, hatua itakayoboresha huduma na hadhi ya uwanja huo kimataifa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dk Emmanuel Nchimbi akiweka jiwe la msingi la uzinduzi wa Jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, leo Januari 16, 2026.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kukamilisha na kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege nchini, ikiwemo kuimarisha huduma za usafiri wa anga wa ndani na kuziunganisha na safari za kimataifa, kwa lengo la kukuza biashara, utalii na kuongeza mapato ya Taifa.
Viongozi, mabalozi pamoja na wananchi mbalimbali wakisikiliza hotuba ya Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi wakati wa uzinduzi wa jengo la viongozi mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere , leo Januari 16, 2026 jijini Dar es Salaam.
Mbali na viwanja vya ndege, amesema Serikali pia imejipanga kuboresha miundombinu mingine ya uchukuzi, kama barabara na reli, ili kuhakikisha huduma za usafiri zinakuwa rahisi na salama.
“Mradi wa barabara za mwendokasi utaendelea na kuunganisha na miundombinu ya ndege ili kuhakikisha usafiri katika miji mikubwa unakuwa wa haraka na wa kisasa,” amesema.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dk Emmanuel Nchimbi akimkabidhi Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa, mfano wa funguo ya Jengo la Viongozi Mashuhuri, wakati wa uzinduzi wa jengo hilo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 16 Januari 2026.
Kwa upande mwingine, ametaja miradi mbalimbali ya kimkakati inayoendelea, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Mbambabay na Kigoma, pamoja na mradi wa Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).
Muonekano wa ndani katika jengo la viongozi mashuhuri lililozinduliwa Januari 16, 2026 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Hii ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo, na hivyo kurahisisha biashara na kuongeza tija katika uchumi wa nchi yetu.
“Uwekezaji katika sekta ya uchukuzi ni gharama kubwa, hivyo ni muhimu kutunza miundombinu hii kwa masilahi mapana ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Muonekano wa ndani katika jengo la viongozi mashuhuri lililozinduliwa Januari 16, 2026 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Kuhusu jengo hilo lilozunduliwa Dk Nchimbi kuwa majengo kama hayo yanapaswa kutunzwa na kuwa na ubora wa hali ya juu ili kutoa picha nzuri ya Tanzania kwa wageni.
“Mamlaka ya Ndege inapaswa kuhakikisha majengo haya yanatunzwa na kubaki na ubora wake,” amesema Dk Nchimbi.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amezungumza kuhusu mafanikio ya mradi wa uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, akisema ni sehemu muhimu ya jitihada za Serikali kuboresha miundombinu ya usafiri anga ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuvutia wageni wakubwa.
“Mradi huu utaongeza nguvu katika shughuli mbalimbali za uchumi na pia ni sehemu ya mpango wetu wa kuboresha viwanja vingine katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesema Serikali inaendelea kufanya upembuzi wa maeneo mengine kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya ndege kama vile mikoa ya Njombe na Singida.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Abdul Mombokaleo amesema jengo hilo limewekwa mifumo ya kisasa ya ulinzi na usalama na lina uwezo wa kuhudumia marais watano kwa wakati mmoja,” amesema Mombokaleo.
Muonekano wa jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, leo Januari 16, 2026
Jengo hilo lina kumbi maalumu kwa ajili ya viongozi wakuu, ukumbi wa kusubiri wageni, sehemu za wacheza ngoma, na maeneo ya kunywa kahawa na chai.
Pia, kuna ukumbi wa mikutano na vyombo vya habari, sehemu ya kuegesha magari, na eneo la uoto wa asili na kupanda maua.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema jengo hilo litakuza uchumi wa mkoa wa Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.
“Jengo hili linahakikisha hadhi ya uwanja wetu inakua, na mkoa wa Pwani utafaidika kwa kupokea wageni wengi kutoka Dar es Salaam,” amesema Kunenge.