Dodoma. Wakala wa nishati ya umeme vijijini (REA) umezindua kituo cha kupoozea umeme Mtera kitakachohudumia Mkoa wa Iringa na Wilaya za Kongwa na Mpwapwa ambazo zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kutokana na umbali mrefu wa kusafirisha umeme huo.
Kituo hicho kilichojengwa kwa thamani ya Sh10 bilioni kimejengwa kwa ufadhili kutoka nchi za Norway na Sweden kila mmoja ikichangia asilimia 5ya gharama hadi kukamilika kwa mradi huo.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kituo hicho leo Ijumaa Januari 16, 2026 Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema kuanza kazi kwa kituo hicho kutasaidia hali ya umeme kutengamaa kwenye mikoa ya Iringa na Wilaya za Kongwa na Mpwapwa ambazo zilikuwa zinakabiliwa na changamoto ya kukatika katika kwa umeme mara kwa mara.
Amesema hiyo ilitokana na umbali mrefu wa kusambaza umeme kwenye maeneo hayo kwani umeme uliokuwa unazalishwa Mtera, ulilazimika kusafirishwa hadi kituo cha kuupozea cha Zuzu ambapo ni umbali wa kilomita 150 hali iliyokuwa inasababisha umeme kukatika au kukosa nguvu unapowafikia wananchi.
”Lakini sasa kuzinduliwa kwa kituo hiki inamaanisha kuwa umeme utakuwa unazalishwa na kupoozewa hapahapa, hivyo wananchi wa maeneo ya Iringa na Wilaya za Kongwa na Mpwapwa wataondokana na tatizo la kukatika kwa umeme na umeme mdogo ambalo lilikuwa linakwamisha viwanda vikubwa kufunguliwa kwenye wilaya hizo, kwani walikuwa wanalazimika kufanya kazi usiku ambapo matumizi ya umeme yamepungua,” amesema Ndejembi.
Amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho ni juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wanafikiwa na maendeleo ya kweli kwa kupitia nishati ya umeme ikiwemo uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo ambavyo vinahitaji umeme wa uhakika.
Amesema mpaka sasa vijiji vyote nchini vimefikiwa na umeme kupitia Rea na kwamba vimebaki vitongoji 21,000 pekee nchini kufikiwa na nishati hiyo ambapo hivi karibuni watasaini mkataba wa kupelekwa umeme kwenye vitongoji 9,009 katika kuhakikisha kuwa vijiji na vitongoji vyote vinafikiwa na nishati hiyo.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba amesema Rea imefanya kazi kubwa ya kusambaza umeme vijijini kwani mwaka 2014 ni asilimia saba tu ya vijiji nchini vilikuwa na umeme lakini mpaka sasa ni asilimia 78 ya vijiji vina umeme na hali ya upatikanaji wa huduma hiyo mjini ikiendelea kutengemaa.
Amesema lengo la kuimarisha huduma za umeme nchini ni kuhakikisha kuwa huduma hiyo inakuwa ya uhakika na siyo ya kukatika kila mara, ili wananchi wafanye shughuli zao za maendeleo bila bughudha
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Rea, Hassan Said amesema umeme unaopozwa kwenye kituo hicho umeshaanza kufanya kazi ambapo mkoa wa Iringa unahudumiwa na megawati tatu huku mkoa wa Dodoma ukihudumiwa kwa megawati sita.
Amesema hali hiyo imepunguza muda wa wananchi kukosa umeme kutoka saa 18 kwa mwezi hadi dakika 40 kwa mwezi, hali inayowafanya wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema mkoa wa Dodoma una ziada ya umeme kwani umeme unazalishwa ni megawati 200 lakini matumizi ya mkoa ni megawati 86 na hivyo kuwa na ziada ambayo haitumiki.