Kampuni ya Mwananchi, MSD waingia makubaliano ya kimkakati kuelimisha wananchi

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na Bohari ya Dawa (MSD) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuelimisha na kuhabarisha jamii kuhusu masuala ya afya, sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi, kwa wakati na zenye manufaa kwa ustawi wa wananchi.

Hatua hiyo inalenga kupanua upatikanaji wa taarifa za afya zilizo sahihi na za kuaminika na kuchochea mchango chanya kwa jamii kote nchini.


Makubaliano hayo yamejadiliwa hivi karibuni wakati wataalamu kutoka MCL walipotembelea MSD kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa taasisi hizo mbili, kubadilishana mawazo na kujadili fursa mbalimbali za ushirikiano katika utoaji wa elimu ya afya kwa umma.

Mjadala huo ulifunguliwa na  Mkurugenzi wa Fedha wa MSD, Undule Korosso ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa Kikosi Kazi cha Uendeshaji wa MSD na akiongoza idara ya fedha katika taasisi hiyo pamoja na Mhariri Mtendaji (EE) wa MCL, Mpoki Thompson.

Ziara hiyo imekuja katika kipindi ambacho jamii inazidi kuhitaji taarifa za uhakika kuhusu mifumo ya huduma za afya, upatikanaji wa dawa, na jitihada za Serikali katika kuboresha sekta hiyo.

Katika mazungumzo hayo, pande zote zilisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuwa daraja kati ya taasisi za umma na wananchi, hasa katika kufafanua majukumu ya MSD katika mnyororo wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

Kupitia majukwaa ya MCL ikiwamo magazeti, mitandao ya kidijitali na vyombo vingine vya habari, taarifa kuhusu sera, maboresho na changamoto katika sekta ya afya zinaweza kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa lugha rahisi na inayoeleweka.


Wataalamu wa MCL walieleza, kama chombo cha habari kinachoongoza nchini, kampuni hiyo ina wajibu wa kushirikiana na taasisi muhimu kama MSD katika kutoa taarifa zenye uhalisia, zinazojikita katika takwimu na ushahidi, ili kusaidia jamii kufanya maamuzi sahihi yanayohusu afya zao.

Aidha, walibainisha ushirikiano huo utaongeza ubora wa taarifa za afya zinazochapishwa na kurushwa, huku ukipunguza upotoshaji unaoweza kujitokeza kutokana na taarifa zisizo rasmi.

Kwa upande wake, MSD ilieleza inaona vyombo vya habari kuwa wadau muhimu katika kufanikisha majukumu yake ya msingi ya kuhakikisha upatikanaji wa dawa salama, bora na kwa gharama nafuu kwa Watanzania.

Kupitia ushirikiano na MCL, MSD inaamini itaweza kuwasilisha kwa umma taarifa sahihi kuhusu taratibu zake, mafanikio yaliyopatikana, pamoja na mikakati inayotekelezwa kukabiliana na changamoto katika usambazaji wa dawa.

Ushirikiano huo pia unatarajiwa kufungua milango ya miradi ya pamoja ikiwamo kampeni za elimu ya afya, makala maalumu, vipindi vya uelimishaji na mijadala itakayowashirikisha wataalamu wa afya, watunga sera na wananchi.


Hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala nyeti ya afya, ikiwamo matumizi sahihi ya dawa, kinga dhidi ya magonjwa, na umuhimu wa mifumo imara ya huduma za afya.

Kwa pamoja, tunatumia taarifa kama nyenzo muhimu ya kuleta athari za kijamii na kuchangia maendeleo ya Taifa.