MAMA MARIAM MWINYI ATEMBELEA SHAMBA LA NGANO LA MLEIHA NA KITUO CHA URITHI WA KIHISTORIA SHARJAH

Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam H. Mwinyi, leo tarehe 16 Januari 2026, ametembelea Shamba la Ngano la Mleiha Wheat Farm jijini Sharjah, shamba lenye zaidi ya ekari 2,000 linaloendeshwa kwa kutumia teknolojia za kisasa za kilimo.

Katika ziara hiyo, Mama Mariam alipata fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu kilimo janja (AI Smart Agriculture), ikiwemo matumizi ya vihisi vya udongo vinavyosimamiwa kupitia programu za akili bandia (AI), kituo cha udhibiti, maabara pamoja na kitengo cha utafiti na maendeleo (R&D). Mafunzo hayo yalitolewa na Mtafiti wa Kilimo, Jawahir Mohammed AlAbdool.

Mama Mariam H. Mwinyi alieleza kufurahishwa na mchakato mzima wa uzalishaji wa ngano bora unaotumia teknolojia, akisisitiza dhamira yake ya kuunga mkono na kuendeleza kilimo kinachotumia teknolojia, taarifa sahihi na ubunifu kwa ajili ya maendeleo endelevu ya sekta ya chakula.

Aidha, Mama Mariam H. Mwinyi alitembelea Mleiha Archaeological Centre, moja ya maeneo yenye thamani kubwa ya kihistoria duniani, ambayo ni sehemu ya Faya Palaeolandscape, eneo la Urithi wa Dunia la UNESCO lililoidhinishwa hivi karibuni.

Katika kituo hicho, alipata fursa ya kujionea ushahidi wa makazi ya binadamu wa kale kuanzia enzi ya mawe (takriban miaka 130,000 iliyopita), ikiwemo zana za mawe, mabaki ya makazi ya Neolithic pamoja na makaburi ya zamani, likiwemo kaburi kubwa la Umm an-Nar lenye umbo la duara la takriban miaka 4,000, pamoja na makaburi ya farasi na ngamia yanayoonesha tamaduni za kijamii na mila za mazishi za kale.

Ziara hiyo inaakisi dhamira ya Mama Mariam H. Mwinyi katika kujifunza, kuenzi urithi wa kihistoria na kuhamasisha matumizi ya teknolojia, ubunifu na maarifa kama nguzo muhimu za maendeleo endelevu.