Dar es Salaam. Uchaguzi mkuu wa Uganda umeendelea kuibua mjadala na malalamiko huku matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi yakionyesha Rais Yoweri Museveni anaongoza kwa kura halali zilizohesabiwa hadi sasa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume, Simon Byabakama, Museveni wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), anaongoza kwa kupata kura 14,232 sawa na asilimia 61.7 ya kura halali.
Jumla ya kura halali kwa wagombea wote hadi sasa ni 23,049, huku kura zilizokataliwa zikiwa 796, sawa na asilimia 3.34 ya kura zote zilizopigwa.
Haya ni matokeo ya awali wakati shughuli ya kuhesabu kura ikiendelea na matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa kesho Jumamosi, saa 10 jioni.
Matokeo hayo ya awali yanaashiria kuendeleza utawala wa karibu miongo minne wa Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 81, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 na anayewania muhula wa saba wa uongozi.
Hata hivyo, upinzani umeibuka kulalamikia mwenendo wa uchaguzi huo ambapo mgombea urais wa chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ameeleza hofu ya kufanyika udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupiga kura jana Januari 15, 2026, Bobi Wine alisema uchaguzi umefanyika gizani ili kurahisisha udanganyifu unaokusudiwa, akiwahimiza wananchi wa Uganda kutokata tamaa licha ya mazingira hayo.
Hali ya malalamiko na mvutano huo imetokana na wasiwasi juu ya uadilifu wa mchakato wa uchaguzi kufuatia kasoro kadhaa zikiwemo kuchelewa kuanza katika baadhi ya vituo, hitilafu za mashine za kidigitali na hofu ya kura feki.
Wakosoaji wa mwenendo wa shughuli hiyo wanasema kuchelewa kufunguliwa kwa baadhi ya vituo vya kupigia kura, hitilafu za mashine za kuwatambua wapigakura na kuzimwa kwa mtandao kote nchini humo, kumeathiri uchaguzi na kuvunja ari ya baadhi ya wapigakura.
Kwa mujibu wa tatatibu za uchaguzi huo, vituo vya kupigia kura vilitarajiwa kufunguliwa saa moja asubuhi lakini baadhi vimeripotiwa kuchelewa kwa saa kadhaa kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya kuendeshea shughuli hiyo.
Mbali na kuchelewa kwa vituo kuanza upigaji kura, mashine za bayometric zinazotumiwa kuhakiki wapigakura kwa alama za videole, zimeripotiwa kushindwa kufanya kazi katika baadhi ya vituo.
Wadau kutoka nchini humo wakiwemo viongozi wa upinzani wanasema kwa lengo la kutumia mashine hizo lilikuwa kuzuia udanganyifu, kushindwa kwake kufanya kazi kumezua wasiwasi wa kuwepo udanganyifu.
Kufutia hitilafu ya mitambo hiyo, Tume ya Uchaguzi iliwaelekeza wapigakura kutumia mfumo wa kawaida wa daftari la wapigakura ili kutoathiri ratiba ya shughuli ya upigaji kura.
Inaelezwa kuwa baadhi ya wapigakura walikosa kutambuliwa kwa alama za na kulazimisha kutumia njia ya daftari ambayo baadhi ya wadau wameikosoa kuwa inatoa mwanya wa kufanyika udanganyifu.
Kutokana na changamoto hizo zinazotajwa kuwa katika baadhi ya vituo, wananchi walionekana kukata tamaa na kuondoka kwenye vituo baada ya kukaa kwenye foleni kusubiri kwa muda mrefu.
Mgombea urais wa upinzani, Bobi Wine, ameishutumu Tume ya Uchaguzi na serikali kwa kutumia ucheleweshaji wa mashine na mtandao kuzima kuendeleza sera ya kushusha ari ya ushiriki wa wapiga kura hasa katika ngome za upinzani.
Wine, pia, amelalamika kuhusu ukamataji wa mawakala wa chama chake na kutolewa katika baadhi ya vituo vya uchaguzi kwa nguvu.
“Kukamatwa na kuondolewa kwa nguvu kwa mawakala wetu vituoni kunapunguza haki ya wananchi kushiriki uchaguzi,” amesema Bobi Wine.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Simon Byabakama amekiri kushindwa kufanya kazi kwa mitambo hiyo, akisema imetokana na hitilafu za kiufundi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kuharibika kwa mashine hakuondoi haki ya mtu yeyote kupiga kura na kwamba taratibu za daftari la wapigakura zilikuwa mbadala wake.
Pia alisema kutakuwa na uchunguzi juu ya sababu za mashine kushindwa kufanya kazi ipasavyo, akisisitiza kila mtu kupata haki yake ya kupiga kura.
Kuzimwa kwa mtandao katika siku za kabla na wakati wa uchaguzi, pia, kunaendelea kulalamikiwa kama njia ya kuharibu uchaguzi huo.
Serikali nchini humo ilizima mtandao wa intaneti kote kwa lengo la kudhibiti taarifa za upotoshaji bila kutaja lini huduma hiyo itarejea na imeendelea kuwa hivyo mpaka sasa.
Wanaharakati na mashirika ya haki za binadamu na Umoja wa Mataifa wameikosoa hatua hiyo kama ukiukaji wa haki za msingi za uhuru wa kujieleza na kupata taarifa.
Licha ya malalamiko hayo, shughuli ya kuhesabu kura ilianza mara moja jana jioni baada ya upigaji kura kukamilika huku Tume ikiahidi taratibu zitasimamiwa vyema.
Kuanzia jana jioni, katika baadhi ya maeneo yanayoaminika kuwa ngome za upinzani, wananchi walishuhudia kura zikihesabiwa kwa uwazi, huku umati wa watu ukishangilia kila jina la Bobi Wine lilipotajwa huku taifa likisubiri kwa tahadhari matokeo rasmi.
Tayari Tume hiyo ilishatangaza kuwa shughuli ya kuhesabu kura itakamilika kesho Jumamosi na kumtangaza mshindi wa kiti cha urais ifikapo saa 10 jioni.