Mwaselela akerwa shule kukosa vyoo, aahidi kujenga vipya, akitoa madawati 400

Mbeya. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya ‘MNEC’ Ndele Mwaselela amewataka viongozi kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea jambo linalokwamisha utatuzi wa changamoto kwenye jamii.

Pia, ameeleza kusikitishwa na miundombinu hafifu ya vyoo katika Shule ya Sekondari Malama iliyopo wilayani Mbeya, ambapo ametoa Sh1 milioni kwa ajili ya ukarabati wa vyoo vipya na kugharamia matundu mengine mapya 12.


Akizungumza leo Ijumaa Januari 16, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi madawati na viti 400 shuleni hapo, Mwaselela amesema kiongozi asiye wa mfano hafai, akieleza kuwa falsafa yake ni kufanya kwa vitendo kuwahudumia wananchi wote.

Amesema kwa shule zilizopo Kata ya Nsalala wilayani humo anapotoka yeye mwenyewe, hataki kuona mzazi au mlezi yeyote akichangishwa chochote kuhusu madawati wala viti.

“Huu ni ubinafsi, hii halihitaji Rais Samia Suluhu Hassan kufika hapa, sasa natoa Sh1 milioni ikarekebishe hiki choo, lakini nataka vijengwe vyoo vingine matundu 12 na gharama ni zangu, kuanzia Jumatatu fundi aanze kazi,” ameagiza Mwaselela na kuongeza;

“Hii haifurahishi wala kufanana na sura zenu, hakuna kuficha mambo kwa karne hii, changamoto inapoonekana, tuitatue, tukifanya hivi tunatengeneza uhusiano wa CCM na wananchi wake,” amesema Mwaselela.


Ameongeza kuwa katika kutekeleza majukumu, viongozi wasiwe na hofu juu ya vyeo vyao, akieleza kuwa baadhi ya viongozi wanashindwa kuongea ukweli kwa sababu ya nafasi zao, akifafanua kuwa kwa kufanya hivyo, safari ya mbinguni itakuwa ndefu.

“Lazima tujikite na matatizo ya wananchi, tufanye kazi kwa uweledi kwa kumuhofia Mungu badala ya cheo, tumekagua vyoo na upungufu upo, mimi nataka vitendo, siyo maneno nafanya hivi kwa niaba ya Rais,” amesema MNEC huyo.

Hata hivyo kiongozi huyo ameahidi kuwa kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne katika shule hiyo, atagharamia malipo ya masomo ya ziada ili kuwasaidia watoto hao kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amesema maelekezo ya Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri, akiwataka watendaji nao kujitolea.

Muonekano wa vyoo vilivyokuwa vikitumika kwa upande wa wavulana katika shule ya Sekondari Malama, ambapo MNEC wa Mkoa huo, Ndele Mwaselela ameahidi kujengwa matundu 12 na kukarabati mengine.



“Tumshukuru Mnec, lakini viongozi wengine tukumbuke maeneo yetu, tusitegemee zaidi Halmashauri kufanya, tuonyeshe uongozi kwa vitendo ili tuboreshe shule zetu, natarajia leo tuko Nsalala, kesho twende kwingine,” amesema Malisa.

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo, Neema Mwakimenya amesema changamoto ya vyoo ni kubwa kwani kwa upande wa wavulana wana upungufu wa matundu 16 pamoja na samani (meza na viti) 673.

Muonekano wa vyoo vilivyokuwa vikitumika kwa upande wa wavulana katika shule ya Sekondari Malama, ambapo MNEC wa Mkoa huo, Ndele Mwaselela ameahidi kujengwa matundu 12 na kukarabati mengine



“Katika upungufu huu, niwashukuru viongozi, Rais na MNEC ambaye ameguswa kwa kiasi kikubwa kutuletea viti na meza kutoka kwake, kwa ujumla viongozi tunawashukuru kwa kila mmoja” amesema Neema.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari wilayani humo, Aliko Mbuba amesema watendaji wataendelea kusimamia vyema elimu, ustawi wa wanafunzi, malezi bora na kuinua taaluma katika shule zote.

“Mahitaji yataendelea kuhitajika kwakuwa idadi inakua, tunafikiria kuanzisha shule nyingine ambapo tukikamilisha hii Malama itakuwa na hadhi ya kuwa na kidato cha tano na sita,” amesema Mbuba.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Aman Yusuph amesema kupatikana kwa vyoo na samani, kutaongeza kujiamini kwa wanafunzi na kuongeza ufanisi katika masomo.

“Zaidi ni kushukuru viongozi wetu kwa kutukumbuka, MNEC anasimamia Mkoa, lakini ameona shule hii inastahili kupata huduma hii, tunaahidi kufanya vizuri kitaaluma na kutunza miundombinu hii,” amesema Yusuph.


Diana Mwakanyamale mkazi wa Nsalala amesema afya ndio msingi wa maisha kwa binadamu na elimu ndio ufunguo wa maisha, hivyo uwapo wa vyoo bora shuleni hapo, inatoa matumaini kwa wazazi kuamini watoto wao wanapata kilicho bora.

“Kuna muda tulikuwa tukija shuleni hapa kwa ujumla mazingira hayakuwa mazuri hadi sisi wazazi tunahofia afya za watoto wetu, alichofanya MNEC leo kimerejesha matumaini,” amesema Diana.