Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Februari 16, 2026 kwa ajili ya upande wa Jamhuri kuwasomea hoja za awali (PH) askari Polisi wawili wanaokabiliwa na mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp wa Mange Kimambi.
Hatua hiyo ni baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni WP 10427 Koplo Vailety Ibrahimu na H 2620 Koplo Thomas Tadei.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kuchapisha taarifa za uongo kwa kutumia kompyuta kupitia mtandao wa WhatsApp wa Mangekimambi80, wakidai wananyanyaswa na kiongozi wao, pamoja na kusambaza taarifa hizo za uongo.
Tarehe hiyo imepangwa leo Januari 16, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili hiyo.
Kabla ya kupanga tarehe hiyo, Wakili wa Serikali, Christopher Olembille, aliieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na kwamba ilipangwa leo kusomewa PH, lakini hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Hassan Makube hayupo, hivyo aliomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine.
Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Mwankuga na kuahirisha kesi hadi Februari 16, 2026.
“Washtakiwa, hakimu anayesikiliza kesi yenu leo mahakamani hapa yupo kwenye mkutano, hivyo mtakuja Februari 16, 2026 kwa ajili ya kusomewa maelezo na kesi itaanza kusikilizwa ushahidi,” alisema Hakimu Mwankuga na kisha kuahirisha shauri hilo.
Washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.
Katika shtaka la kwanza, Vailety na Tadei wanadaiwa kuwa Septemba 24, 2025, katika eneo la Kituo cha Polisi Bandari jijini Dar es Salaam, walichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp wa Mangekimambi80, wakidai wananyanyaswa na kiongozi wao.
Inadaiwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kudanganya umma, huku wakijua si kweli.
Shtaka la pili ni la kusambaza taarifa, ambapo katika tarehe hiyo na eneo hilo, washtakiwa wanadaiwa kusambaza taarifa hiyo iliyohusiana na usalama wa taifa bila kuwa na kibali kutoka mamlaka husika.