Profesa Kitila atangaza vita na wanaoomba rushwa wawekezaji

Dar es Salaam. Serikali imesema inatambua uwepo wa baadhi ya watumishi wanaosumbua wawekezaji kwa kuwaomba rushwa pindi wanapokuja nchini, huku ikiahidi kuwashughulikia.

Hilo linawekwa wazi wakati ambao kampeni maalumu ya kuvutia uwekezaji wa ndani katika mwaka 2026 inazinduliwa, ikilenga kuongeza ushiriki wa wazawa katika uwekezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kampeni hiyo imezinduliwa leo Ijumaa, Januari 16, 2026 huku ikitarajiwa kufika mikoa yote nchini wakati ambao Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza) imepewa lengo la kusajili miradi 1,500 kwa mwaka 2026.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema wakati nchi ikijivunia mafanikio katika uwekezaji yaliyoshuhudiwa ndani ya miaka mitano, bado kuna vitu vinapaswa kufanyiwa kazi.

Suala la kutokomeza rushwa ni moja ya jambo ambalo wataliangalia wakati wakifanya maboresho ya mazingira ya biashara sambamba na kupunguza udhibiti uliopita kiasi.

“Rushwa, tunajua bado kuna watu wetu wachache ambao rushwa kwao wana mapenzi nayo wanasumbua wawekezaji wetu.

Nina kesi zimeletwa kwenye baadhi ya sekta hata huko uwanja wa ndege wanapoingia watu wetu, bado hiyo hali ni changamoto,” amesema.

Amesema kama Serikali itahakikisha inakomesha suala hilo ili kuweza kuboresha huduma zinazotolewa kwa wawekezaji huku zikifuata sheria na kanuni na taratibu.

Ili kufanikisha hilo, tayari mapitio ya sheria na mkakati unaolenga kuboresha uwekezaji umekamilika ili kuboresha mazingira ya uwekezaji yanayoweza kuvuta mitaji yandani na nje ya nchi.

“Kazi kubwa imefanyika lakini bado tunataka kufanya zaidi ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira 2050 kwani

Tunataka watu wakija kuwekeza wafanye hivyo kwa haraka bila vikwazo,” amesema.

Profesa Mkumbo amesema hayo yote yanafanyika kwa sababu hakuna nchi inayoweza kufikia maendeleo ya hali ya juu bila ushiriki wa wazawa katika uchumi wake, na vivyo hivyo, hakuna uchumi unaoweza kukua kwa kasi bila kuvutia na kushirikisha uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi.

“Ukiona Taifa kubwa kama China na Marekani wanapambana kuvuta wawekezaji kutoka nje sisi ni nani tusifanye hivyo. Wakati mwingime wakiona watu wanakaribisha watu wanasema unaona wanapewa watu wa nje wakati sisi tupo, ndiyo maana tumekuja na kampuni hii ili kila mmoja ashiriki kwenye uwekezaji,” amesema.

Kufuatia hilo ndiyo maana wameamua kuvutia wawekezaji wa ndani pia kwa kuwapatia elimu na kubadili mtazamo wa Watanzania unaowafanya washindwe kuelewa dhana ya uwekezaji wakidhani ni jambo la watu wenye hela nyingi kutoka nje.

“Kila mtu anaweza kuwa mwekezaji ikiwa unaanza kuwekeza kidogokidogo kupitia kuweka akiba na kuweka mipango kwa ajili ya miaka ijayo. Kuwa mwekezaji si lazima uwe tajiri mkunwa bali hata wenye kipato kidogo unaweza kuwekeza badala ya kuwa na suti 20 unakuwa nazo mbili nyingine zinafanya mambo mengine,” amesema

Kuhusu uwekezaji nchini, Profesa Mkumbo amesema wamejitahidi kuutenganisha na masuala ya kauli au misimamo ya kisiasa na ili kufanikisha hilo Tiseza imepewa mamlaka makubwa ya kufanya maamuzi.

“Sasa Tiseza ina uwezo mpana zaidi wa kutekeleza majukumu yake bila vikwazo vya awali. Nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara umuhimu wa kituo hiki, hususan katika kutoa huduma kwa wawekezaji na kushughulikia masuala yao kwa ufanisi. Leo, kituo hiki kina uwezo na hadhi kubwa zaidi,” amesema.

Kwa kufanya hivyo, wawekezaji watakuwa na uhakika wa kisheria na usalama wa uwekezaji wao, kwa misingi ya sheria huku wakijenga mazingira ambayo maamuzi yanafanyika kwa haki, kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria, ili wawekezaji wawe na imani na mifumo ya kisheria na kiutawala.

“Tukisikilizana kwa dhati, tunasikiliza pia mahitaji ya kila upande, kwa sababu ni kweli kwamba hata Serikali ina changamoto zake, hususan katika masuala ya takwimu na mapato. Ndiyo maana njia bora ya kushughulikia masuala haya ni kupitia ushirikiano wa moja kwa moja, si kupitia mitandao ya kijamii. Changamoto nyingi zina mizizi ya pamoja, na suluhisho lake pia ni la pamoja,” amesema.

Mkurugenzi wa benki ya Equity, Isabela Maganga amesema huu ni wakati muafaka na sahihi kwa nchi kuendelea kuwekeza na kupanua uwekezaji kutokana na mazingira mazuri ya kiuchumi yaliyopo.

Katika muktadha huu, Benki ya Equity wanashirikiana na sekta mbalimbali, si kwa sababu tu wana mtaji mkubwa wa kufadhili uwekezaji bali kwa sababu wana mkakati madhubuti wa kibiashara na kimasoko wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha uwekezaji katika nchi zote tunazofanya kazi.

“Hii ndiyo sababu tunaamini kuwa ni lazima tushirikiane kwa karibu na sekta husika. Tumejipanga kikamilifu na tumejizatiti kusaidia uwekezaji kukua hapa Tanzania na endapo mtapenda kupanua biashara zenu kuvuka mipaka, tuko tayari kuwaunga mkono,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Deogratius Massawe amesema mkutano huo ni moja ya jambo litakalosaidia kutimiza Ajenda ya Dira ya 2050.

Dira hii inatambua wazi nafasi muhimu ya sekta binafsi kama mhimili mkuu wa maendeleo ya Taifa.

“Tunatambua hatua na maendeleo ambayo Serikali imepiga katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, licha ya changamoto chache zilizopo. Mwitikio huu wa dhamira na mazungumzo endelevu hautapunguza tu gharama za kufanya biashara, bali pia utatukaribisha zaidi katika kufikia malengo ya Dira ya 2050,” amesema.

Kufuatia hilo amesema wako tayari kuunga mkono michakato ambayo tayari imeanzishwa.

“Kwa upande wetu, tunahitaji mazingira ya uwekezaji yaliyo thabiti na yanayotabirika ili kusaidia maendeleo ya muda mrefu. Hatutazami tu siku zijazo tunalenga ushirikiano wa kudumu na maboresho endelevu katika uhusiano kati ya sekta binafsi na serikali. Kwa kufanya kazi kwa pamoja, bega kwa bega na Serikali, tuna imani kuwa tutaweza kufanikisha dira hii,” amesema.