Sita washikiliwa tuhuma za mauaji ya bodaboda Ngosha Tabora

Tabora. Watu sita wamekamatwa mkoani Tabora kwa tuhuma za mauaji ya waendesha bodaboda akiwemo Hamisi Nchambi maarufu Ngosha ambaye mwili wake ulitelekeza juu ya kaburi.

Hatua hiyo imekuja baada ya operesheni ambayo imeendeshwa na Jeshi la Polisi mkoani Tabora kutokana na matukio ya mauaji ya bodaboda.

Akizungumza leo Ijumaa Januari 16, 2026, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi amesema wakati wa mahojiano ya awali watuhumiwa wote wamekiri kuhusika na mauaji ya bodaboda waliouawa hivi karibuni.

Amesema mahojiano ya kina yanaendelea ili kubaini matukio mengine zaidi endapo watakuwa wameshiriki au kutambua mnyororo mzima wa uhalifu ili kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Aidha kufuatia operesheni ambayo imefanyika katika wilaya za Uyui, Nzega, Urambo na Kaliua mkoani Tabora watuhumiwa wanne wamekamatwa wakiwa na mashine Tatu, vikatia chuma viwili (Grender), nyaya mbili za grender hizo na hydrolic lita 40,ambapo vitu hivyo vimeibiwa katika mradi unaoendelea kutekelezwa wa Ziwa Victoria.

Pikipiki iliyoporwa mara baada ya kuuawa bodaboda Hamisi Nchambi maeneo ya makaburini Malolo, Tabora.



“Watu hawa wameiba hivi vitu na baadaye wakaenda kuvificha katika kitongoji cha Ubalani na Majengo wilayani Urambo mkoa wa Tabora,” amesema.

Katika tukio jingine amesema Jeshi la Polisi limewakamata watu watano kwa tuhuma za wizi wa pikipiki pamoja na pikipiki tisa ambazo zimeibiwa katika wilaya ya Nzega mkoani Tabora na Kahama mkoani Shinyanga na kwamba watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kufuatia matukio hayo maofisa usafirishaji Tabora maarufu bodaboda wameandamana kwa amani mpaka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora ili kujua ni lini matukio ya mauaji ya bodaboda yatakomeshwa kikamilifu.

Kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Tabora, mkuu wa wilaya ya Tabora, Upendo Wella amesema vyombo vya ulinzi vinaendelea na operesheni zake kuhakikisha watu wote wanakuwa salama na asiwepo mtu wakutishiwa amani na mtu mwingine kama ambavyo imeshuhudiwa kwa bodaboda waliopoteza maisha.

“Sisi tupo kwa ajili ya kuhakikisha mnaishi salama mkiendelea na majukumu yenu na si vinginevyo hivyo ikitokea mtu anavunja sheria lazima tuchukue hatua kali kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Kuhusu utekelezaji wa ulinzi kwa wananchi, Kamanda Mbogambi amesema Jeshi la Polisi linafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanakomesha vitendo vyote vya kihalifu mkoa wa Tabora na kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria.

“Haiwezekani eti watu wachache wasumbue watu hapa mara waue wenzao na kuchukua piki piki hatuwezi kucheka na watu wa sampuli hii,” amesema.