TUME YA TEHAMA KUWAKUTANISHA WADAU WA TEHAMA NCHINI

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt Nkundwe Mwasaga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam

……………..

Tume ya TEHAMA nchini inatarajia kuwakutanisha watumiaji wa Tehama wa ndani na nje ya nchi katika Kongamano la kujadili mapinduzi ya kidigitali katika Dira ya mwaka 2050.

Akizungumza leo na wanahabari jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt Nkundwe Mwasaga amesema kuwa kongamano hilo ni la Tisa kufanyika nchini ambapo litaanza Januari 19 mpaka 23 mwaka huu.

Dkt Mwasaga amesema kuwa watajadiliana masuala mbalimbali yanayohusiana na mapinduzi ya kidigitali ambayo kwenye Dira itasaidia kufikisha kwa haraka uchumi wa Trilioni 1 za kimarekani mwaka 2050.

“Maana kubwa ya kukutana kwenye kikao hiki ni kujianda kujadiliana na kuwasikiliza wataalamu wetu wa ndani,kampuni changa,wataalamu kutoka nje zikiwemo kampuni binafsi ili kujadiliana kwa pamoja mambo ya kufanya katika miaka 25 ijayo’amesema Dkt Mwasaga

Dkt Mwasaga amesema kuwa katika kongamano zitajadiliwa mada mbalimbali ikiwemo inayohusu vijana pamoja na wanawake katika mapinduzi ya kidigitali.

Aidha amezitaja nguzo tano za matumizi ya kidigitali kuwa ni pamoja na ujuzi wa kidigitali,wataalamu wa kati na watu wenye ujuzi wa juu wa kidigitali utakaowasaidia kutengeneza mifumo mahususi inayotumia Akili Unde ili kufikisha huduma mahususi kwa watu.

Ameendelea kusema kuwa katika kongamano hilo ni kuangalia usalama wa mitandao mbalimbali ikiwemo ulinzi wa faragha za watu,taarifa binafsi na kuweza kumlinda mlaji.

Hata hivyo Dkt Mwasaga amesisitiza
kuwa kongamano hilo ni mahususi kwa ajili ya kujadili Dira ya mwaka 2050 na
kujiandaa kwa wataalamu wa TEHAMA pamoja na wananchi wote wanaotumia mitandao
katika shughuli zao za kila siku, jambo litakalosaidia kuanza utekelezaji wa
dira hiyo kuanzia Julai 1, 2026 kwa ufanisi mkubwa 
hivyo
amewasisitiza watanzania kutumia fursa ya kongamano hilo ili kujadili masuala
mbalimbali ya kidigitali