Vigogo walivyogawana kamati za Bunge

Dar es Salaam. Bunge la 13 limeunda kamati 17 za kiseta huku waliokuwa mawaziri kwa nyakati tofauti wakitawanywa kwenye kamati mbalimbali.

Tayari kamati hizo zimekaa na kuwachagua viongozi wake, wenyeviti na makamu wenyeviti na jana Jumatano Januari 14, 2026 Ofisi ya Bunge ilitangaza majina ya vigogo hao.

Kamati mbili kati ya hizo zinaongozwa na wabunge wa upinzani kwa mujibu wa kanuni, ambao ni Devotha Minja (Chaumma), anayeongoza Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Ado Shaibu (ACT Wazalendo) Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Katika mgawanyo unaohusisha wabunge wote ambao si mawaziri, Spika wa zamani wa Bunge, Dk Tulia Ackson na mawaziri wa zamani Nape Nnauye na Dk Seleman Jafo wamepangwa kwenye kamati moja ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama

Wengine katika kamati hiyo ni Omary Kipanga, Elibariki Kingu, Mary Chatanda (mwenyekiti UWT) na Christina Mndeme (aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu CCM, Bara).

Kamati hiyo inaongozwa na Najma Giga, aliwahi kuwa meenyekiti wa Bunge kwa nyakati tofauti.

Aidha, mawaziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Kilimo na Maliasili na Utalii, Innocent Bashungwa, Japhet Hasunga na Dk Pindi Chana nao wamepangwa katika kamati moja ya Bajeti, ambayo mwenyekiti wake ni Mashimba Ndaki, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Vigogo wengine waliowekwa kamati moja ya Miundombinu itakayoongozwa na Seleman Kakoso, ni Profesa Joyce Ndalichako (Waziri wa zamani wa elimu) na Hussein Bashe (Waziri wa zamani wa Kilimo).

Hata hivyo, jina la Profesa Ndalichako limechomoza pia katika Kamati Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo mwenyekiti wake ni Anne Kilango Malecela na makamu wake ni Christina Mndeme.

Mbunge wa Bukombe (CCM) na aliyekuwa naibu waziri mkuu, Dk Doto Biteko amepangiwa Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo, itakayoongozwa na Husna Sekiboko akisaidiana na Cornel Magembe.

Waziri wa zamani wa Mifugo, Dk David Mathayo na Philip Mulugo (Naibu waziri wa elimu wa zamani) na mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ wamepangwa katika Kamati ya Madini, inayongozwa na Subira Mgalu.

Sambamba na hao, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene na mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chiponda ‘Babalevo’ wamepangwa katika Kamati ya Sheria Ndogo, chini ya uenyekiti wa Cecilia Pareso.

Naye, Waziri wa zamani wa Nishati, Profesa Sospeter Muhongo, mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete (ambaye ni Mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete), Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ wamepangwa katika Kamati ya Viwanda, Biashara na Kilimo, inayongozwa na Deodatus Mwanyika.

Pia, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amepangwa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, huku Jesca Magufuli (mtoto wa rais wa awamu ya tano-hayati John Magufuli) akipangwa kamati ya Tamisemi.

Hata hivyo, taarifa ambazo Mwananchi limedokezwa ni kwamba baadhi ya wabunge wamewasilisha maombi kwa Spika Mussa Zungu ili kubadilishiwa kamati.

“Kuna wabunge wameomba kwa Spika kubadilishiwa kamati na kamati hizi zinapangwa na Spika, sasa anaweza kuwabadilisha ama akawaacha hapohapo hilo litategemea sasa na uamuzi wa Spika mwenyewe,” kimesema chanzo chetu kikiomba hifadhi ya jina.

Akizungumzia mgawanyo wa wajumbe katika kamati hizo, mchambuzi wa siasa na jamii, Ali Makame amesema baadhi ya wajumbe wa kamati hizo waliowahi kushika nyadhifa za juu, hivyo watangulize uzalendo.

“Katika siasa kitu kinachoweza kukusogeza mbele ni uvumilivu, hasa ukisoma alama za nyakati. Wengi wao bado umri unawaruhusu kufika mbali zaidi katika siasa,” amesema.

“Msingi wa mafanikio ya uongozi ni kuwa na uvumilivu pale unapopanda na kushuka. Kikubwa angalia msimamo ulionao na malengo katika kulitumikia Taifa,” amesema Makame.

Kwa mujibu wa Makame, mtu au kiongozi akitangulia ubinafsi mbele hawezi kufika popote kimaendeleo, lakini uzalendo mbele wa kutambua muda na wakati unaweza kuwekwa popote utafanikiwa.

“Kubaliana na mabadiliko, lakini ukichunga maadili ya uongozi utafika mbali.Waliokuwa mawaziri wasishtuke wala kuhuzunika, kwamba mimi nilikuwa nafasi ya juu, lakini leo nipo kwenye kamati,”

“Unapokuwa katika kamati ni msimamiaji wa yale majukumu unayopangiwa na kamati husika.Cha msingi waendelee kuwa waadilifu, uzalendo na kuheshimu miiko ya uongozi ili kufika mbali,” amesema Makame.

Makame amesema ikitokea kiongozi umesahau malengo ya uongozi au ya chama chako, basi kuna uwezekano ukaligawa Taifa vipande vipande.