Vijana 5,746 wachaguliwa mafunzo ya uanagenzi, Serikali yasisitiza ajira na ujuzi kwa vitendo

Dodoma. Serikali imetangaza kuwa jumla ya vijana 5,746 wamechaguliwa kujiunga na mafunzo ya uanagenzi kati ya 20,247 waliomba kushiriki kwa mwaka wa mafunzo 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taifa za kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa vitendo na kuongeza fursa za ajira nchini.

Akizungumza leo Ijumaa, Januari 16, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Deus Sangu amesema baada ya mchakato wa uhakiki kukamilika, vijana hao wamechaguliwa kuanza mafunzo hayo kuanzia Januari 19, 2026.

Kwa mujibu wa Waziri Sangu, majina ya vijana waliochaguliwa pamoja na vyuo watakavyopangiwa yatatangazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu (www.kazi.go.tz), pamoja na magazeti na mitandao ya kijamii kuanzia Januari 17, 2026.

Aidha, amesisitiza mafunzo hayo yatatolewa bila malipo, huku Serikali ikigharamia asilimia 100 ya gharama za mafunzo.

Amewataka wazazi na walezi kuwahimiza vijana wao kuchangamkia fursa hiyo muhimu ya kujijengea ujuzi na mustakabali wa ajira.

“Tunawahimiza vijana wote waliopata nafasi ya kushiriki mafunzo haya kuripoti katika vyuo walivyopangiwa kwa wakati, kwa kuzingatia nidhamu, bidii na kufuata sheria na taratibu za vyuo,” amesema Waziri Sangu.

Kwa upande mwingine, Serikali imeeleza jumla ya vyuo 103 vilihusishwa katika mchakato wa awali wa kutoa mafunzo ya uanagenzi, ambapo baada ya tathmini, vyuo 47 vilithibitishwa kuendelea kutoa mafunzo hayo katika fani mbalimbali zikiwemo uashi, useremala, umeme wa majumbani na viwandani, ufundi magari, uchomeleaji, uchongaji vyuma, Tehama, huduma za hoteli na utalii pamoja na madini.

Waziri Sangu ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha programu hiyo, akisisitiza kuwa kukuza ujuzi kwa vijana ni msingi wa maendeleo ya taifa na uchumi jumuishi.

Akiozungumzia mafunzo hayo, Rehema Mwakalukwa, mkazi wa Chang’ombe, Dodoma, amesema mafunzo ya uanagenzi yatawasaidia vijana kujitegemea mapema.

“Si kila kijana anaweza kufika chuo kikuu, lakini kupitia uanagenzi anaweza kupata ujuzi na kujiajiri au kuajiriwa. Huu ni mpango mzuri sana,” amesema.

Kwa upande wake, Martin Zakaria, fundi majeneza jijini Dodoma, ameitaka Serikali kuongeza idadi ya wanaonufaika kila mwaka.

“Waombaji ni zaidi ya 20,000 lakini wanaochaguliwa ni chini ya elfu sita. Tunaomba fursa hizi ziongezwe ili vijana wengi zaidi wapate ujuzi,” amesema.