‘Wanafunzi Simanjiro wasizuiwe kisa sare hata wavae rubega’

Simanjiro. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro (DC), mkoani Manyara, Fakii Lulandala amewaagiza walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, kutowazuia kuanza masomo wanafunzi wasiokuwa na sare za shule.

Shule za msingi na sekondari nchini zimefunguliwa Januari 13, 2025 huku wanafunzi wapya wakianza masomo yao kwa darasa la kwanza wa shule za msingi na kidato cha kwanza kwa sekondari.

Lulandala akizungumza Januari 16, 2026 amesema wanafunzi wasizuiwe kuanza masomo yao wasipokuwa na sare wapokelewe hata kama wamejifunga mashuka ya asili (rubega).

Amesema suala la sare za shule litakuja baadaye ila kwa sasa umuhimu unaotakiwa ni wanafunzi kuhudhuria shuleni na kuanza masomo yao kwenye shule za msingi na sekondari.

“Mwanafunzi asiye na sare asirudishwe kabisa hata mmoja apokelewe endapo amevaa rubega pia ajiunge na shule wazazi na walezi watanunua nguo za shule wakianza masomo,” amesema.

Ameeleza kwamba lengo ni kuhakikisha asilimia 100 ya wanafunzi wote wanaopaswa kujiunga na elimu ya msingi na sekondari wanafika shule.

Hata hivyo, amewaagiza wazazi na walezi watimize wajibu wao na kutoipa mzigo serikali kwa kisingizio cha elimu bure.

“Suala la elimu bure halipo ila kuna elimu bila malipo japokuwa majukumu ya serikali yapo yanafahamika na ya mzazi yanaeleweka,” amesema DC Lulandala.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota ameahidi kusimamia utekelezaji wa agizo hilo la mkuu wa wilaya.

Makota ameeleza watahakikisha wanafuatilia wanafunzi wote wafike shule kwa asilimia 100 kama mwaka uliopita wa 2025.

Mkazi wa kata ya Orkesumet, Esupaat Daniel amepongeza juhudu za mkuu huyo wa wilaya katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu.

Esupat ameeleza mwaka jana wazazi na walezi walipeleka watoto wao mashuleni wakihofia kuchukuliwa hatua kali na serikali.

Amesema hata wazazi na walezi waliokuwa na tabia ya kuozesha watoto wadogo kwa tamaa ya kupewa madume ya ng’ombe waliacha kwa kuhofia Serikali.