Tanga. Uongozi wa Chama cha Wavuvi Mkoa wa Tanga umetangaza kusitisha mgomo wa kusitisha shughuli za uvuvi uliokuwa umeanza kwa muda usiojulikana, baada ya serikali kukubali kuwapa wavuvi muda wa kujisajili kwenye mfumo mpya wa ulipaji wa leseni kwa njia ya kielektroniki.
Akizungumza na Mwananchi Januari 16, 2026 Mwenyekiti wa chama hicho, Bombea Salimu, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya serikali kusikiliza kilio cha wavuvi waliokuwa wakilalamikia ugumu wa kujiunga na mfumo mpya wa TAI kutokana na ukosefu wa nyaraka muhimu.
Salimu amesema baada ya mgomo wa siku mbili mfululizo, serikali imekubali wavuvi walipe leseni zao kwa awamu hadi mwezi Machi, huku wakiendelea kushughulikia upatikanaji wa nyaraka muhimu ikiwemo namba ya NIDA, cheti cha kuzaliwa na namba ya mlipakodi (TIN).
“Changamoto kubwa ni kwamba wavuvi wengi hawana taarifa muhimu za kujiandikisha kwenye mfumo. Walipoona zoezi la ukaguzi na ‘kamata kamata’ linaanza, wakaamua kugoma kuingia baharini. Hawakatai kulipa leseni, wanahitaji tu kupewa muda wa kujiandaa,” amesema Salimu.
Amefafanua kuwa katika mfumo wa awali, wavuvi walikuwa wakilipa Sh20,000 na wachuuzi Sh15000 na taratibu za kupatiwa leseni zilikuwa zikifanyika mara tu unapolipa, tofauti na mfumo mpya unaowalazimu kuwa na nyaraka zote kabla ya kusajiliwa.
Salimu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa huduma zimeanza kurejea katika soko la samaki, na kuwataka wafanyabiashara wa ndani na nje ya Mkoa wa Tanga kurejea kuchukua samaki kama kawaida baada ya hali kutengemaa.
Shuguli za ununuzi na uuzaji wa samaki kwenye soko la Kasera jijini Tanga mara baada ya kusitishwa kwa siku mbili mfululizo kufuatia mgomo wa wavuvi.
Kwa upande wake, Mjata Bakari, mjumbe wa Chama cha Wavuvi Mkoa wa Tanga, ameishukuru serikali kwa kusikiliza malalamiko yao, akisema hatua hiyo itawawezesha wavuvi kuendelea na shughuli za uzalishaji, kujipatia kipato na kulipa kodi kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Naye Bakari Hamis Bakari, kiongozi wa manahodha katika eneo hilo, amesema mgomo huo uliwaathiri kiuchumi kwa kiwango kikubwa kwa kuwa wavuvi wengi wanategemea uvuvi kama chanzo chao kikuu cha maisha.
“Hakuna aliyependa kugoma, lakini haikuwa rahisi kuendelea kufanya kazi bila suluhu. Ilibidi tugome ili sauti yetu isikike,” amesema.
Kwa upande wa wachuuzi wa samaki, Zimamu Salehe, amesema maisha yao yanategemea moja kwa moja shughuli za wavuvi.
“Wavuvi wakienda baharini nasi maisha yanakuwa mazuri. Siku mbili za mgomo tulikosa cha kufanya, hata fedha ya chakula ilikuwa changamoto,” alisema.
Mchuuzi mwingine, Kubo Kassi Kubo, alisema hawatamani tena kushuhudia mgomo kama huo, akisisitiza kuwa wachuuzi ndio waathirika wa kwanza wa hali hiyo.
“Soko hili ndilo linatulisha sisi na familia zetu. Mgomo ukitokea, njaa inatugusa kwanza,” amesema.
Wachuuzi wa samaki soko la Kasera jijini Tanga waki endelea na shuguli zao mara baara ya kusitishwa kwa mgomo wa wavuvi.
Akizungumzia hali ya usajili, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Sebastian Danda, amesema hadi sasa ni wavuvi 50 pekee kati ya zaidi ya wavuvi 1,500 waliopo eneo hilo ndio waliosajiliwa, hali iliyosababisha serikali kuanza kuchukua hatua za kuhamasisha ulipaji wa leseni.
Mgomo huo umeathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa samaki katika Jiji la Tanga na baadhi ya maeneo ya nje ya Mkoa wa Tanga yanayotegemea soko hilo kama chanzo kikuu cha kitoweo cha samaki.