Wavuvi walalamikia uvamizi Ziwa Victoria, Serikali yachukua hatua

Rorya. Wavuvi katika Kata ya Bukura wilayani Rorya, mkoani Mara wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kukomesha vitendo vya uvamizi vinavyofanywa na wavuvi kutoka nchi jirani ya Kenya kwenye eneo lao ndani ya Ziwa Victoria.

Wavuvi hao wametoa ombi hilo  Alhamisi Januari 15, 2026 katika Kijiji cha Kirongwe wilayani Rorya walipokuwa wanatoa kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi aliyefanya ziara kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Wamesema changamoto ya uvamizi katika eneo hilo imedumu kwa muda mrefu na imekuwa ikiwaathiri, kiusalama, kiuchumi na kijamii, hivyo ipo haja ya Serikali kuingilia kati na kutafuta suluhisho la kudumu ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na tija.

Samson Ayoma, mmoja wa wavuvi hao amesema changamoto hiyo imedumu  kwa zaidi ya miaka 30 ambapo wavuvi kutoka nchi hiyo wamekuwa wakivamia na kuwanyang’anya samaki na wakati mwingine huchukuliwa mashine na mitumbwi yao, jambo linalowarudisha nyuma katika mapambano dhidi ya umasikini.

“Kinachotushangaza ni kwamba hawa watu hawakamatwi, wakifika wanafanya uhalifu wao na kuondoka, tumechoshwa na hali hii tunaomba kamati yako ya ulinzi usalama itusaidie kabla hatujachukua hatua zingine kisha tukalaumiwa,” amesema.

Jonathan Mahanda anasema mbali na kuchukua mali zao, wavuvi hao wamekuwa na tabia ya kufanya shughuli zao ndani ya eneo la Tanzania, kinyume cha sheria shughuli ambazo wakiwa na silaha za moto.

Amesema hali hiyo imekuwa ikiwapa hasara kwani wao wanalazimika kulipa ushuru na tozo zingine, lakini wanaonufaika ni watu wengine.


Amemwomba mkuu huyo wa mkoa kufanya uchunguzi katika idara ya uvuvi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya kwa madai kuwa wapo watumishi wa idara hiyo ambao pia sio waaminifu.

“Sisi tuna utaratibu wa kufunga ziwa kwa muda wa wiki mbili kila mwezi, ili kuruhusu samaki kuzaliana wenzetu kule hawana utaratibu huo na kibaya zaidi wakati tukiwa tumefunga wao wanakuja na kuvua huku kwetu, jambo ambalo pia ni hatari kwa ukuaji na uendelevu wa samaki ziwani,” amesema Ezekiel Odero

Kaunda Miso amesema hali hiyo isipodhibitiwa upo uwezekano wa wao  kushindwa kumudu gharama za maisha kwani shughuli za uvuvi ndio shughuli  za kuu za kujipatia kipato na kiuchumi.

“Tumeteseka kwa muda mrefu, tunasomesha watoto na kupata mahitaji yetu kupitia ziwa hili  lakini sasa hatuna amani na hatuwezi kufanya shughuli zetu vizuri, tunaomba msaada wa haraka,” amesema.

Kufuatia madai hayo, RC Mtambi amekiri kuwa na taarifa juu ya uwepo wa changamoto hiyo huku akisema hatua kadhaa zimechukuliwa ili kukomesha vitendo hivyo ili wavuvi waweze kufanya shughuli zao katika mazingira salama.

Kanali Mtambi amesema hatua hizo zimegawanyika katika makundi mawili ya muda mrefu pamoja na za muda mfupi ambapo amefafanua kuwa ili kupata suluhisho la kudumu, Serikali inatarajia kujenga kiteule cha jeshi kwa upande wa wana maji katika maeneo hayo yaliyoathirika.

“Novemba mwaka jana Mkuu wa Majeshi alituma timu yake kufanya utafiti hapa Sota ili kujenga kituo kiteule cha jeshi wana maji na muda si mrefu kitajengwa na hii itasaidia kuimarisha ulinzi kwa rasilimali ziwa pamoja na wote mnaofanya shughuli zenu ziwani,” amesema

Pia ametoa onyo kwa wale wote wanaofanya uhalifu majini hasa wanaovamia upande wa Tanzania na kufanya uvuvi wakati ziwa limefungwa kwa maelezo kuwa hali hiyo haikubaliki  na wakikamatwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Amemuagiza Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya na timu yake kufanya vikao vya ujirani mwema na viongozi wa usalama kwa upande wa Kenya ili kukomesha mwingiliano wa masuala ya ulinzi kutoka nchi jirani ndani ya ziwa hilo.

Pia amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Rorya kuongeza doria ziwani ili kuhakikisha wavuvi wanakuwa salama na mali zao muda wote sambamba na ziwa kwa ujumla.

“Hili  kuvua samaki wakati sisi tumefunga ziwa ni uhujumu uchumi, haiwezekani wewe umetunza chakula chako kwaajili ya matumizi yako baadaye halafu jirani anakuja na kuchukua, hii haikubaliki, hatuwezi kukubali kuchezewa kiasi hiki, lazima watu wakamatwe na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria zetu,” amesisitiza