Waziri Makonda aenda Morocco kuzifuata fainali za AFCON 2027

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ameondoka nchini leo Januari 16, 2026 kwenda Morocco tayari kwa ajili ya kupokea kijiti cha maandalizi ya Kombe la Mataifa (AFCON) 2027.

Tanzania ni mojawapo ya nchi wenyeji rasmi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ikishirikiana na Kenya na Uganda kupitia mpango wa ‘Pamoja Bid’ ambapo amesema mara baada ya kukabidhiwa kijiti hicho Januari 18 mapema siku inayofuata wanaanza maandalizi.

Akizungumza na waandishi wa habari saa chache kabla ya kuondoka nchini,  Makonda amesema ameondoka na mambo matatu muhimu aliyoagizwa na Rais Samia Suluhu kwa lengo la kuhakikisha wanajifunza mengi kupitia waandaaji wa mwaka huu.

“Rais Samia amedhamiria kwa dhati kuiweka Tanzania katika ramani ya Dunia katika michuano yote ameniagiza Morocco kuhakikisha naenda kujifunza mambo mbalimbali ambayo yataisaidia nchi kuingia kwenye historia kupitia mashindano hayo.”

Akitaja mambo hayo matatu, Makonda amesema jambo la kwanza ni kumpelekea barua Rais wa CAF, Dk Patrice Motsepe kwa ajili ya shukrani ya kutambua kuhudi za rais wa nchi kuwekeza katika michezo na uwekezaji wa miundombinu.

Amesema jambo la pili wanaenda kujifunza mbinu kutoka Morocco namna watakavyoweza kutumia wenyeji wao kuhakikisha timu ya taifa, Taifa Stars inabaki na kombe nyumbani na jambo la tatu namna ya kutumia michuano hiyo kupaa kiutalii kama ilivyo nchi hiyo ambayo inashika nafasi ya kwanza.

“Morocco inashikilia namba moja kwa utalii, lakini kimichezo ni namba moja, hivyo kujifunza kutoka kwao sio vibaya, kwani tunataka kupitia uenyeji huu tuweze kutoa ajira nyingi kuanzia huduma za usafiri, vyakula, hoteli ili michuano hiyo kutokana na hadhi yake iache historia katika nyanja nyingi.”

Lakini Makonda amesema kwa upande wa burudani wanatarajia kushindanisha wasanii kuandaa wimbo bora utakaotumika katika michuano hiyo, hivyo hivyo kwa vikundi vya ngoma.

“Milango ipo wazi kwa Watanzania wote kutoa maoni kwa wizara katika kile wanachoamini kinaweza kuwa chachu ya kuboresha au kuhamasisha michuano hiyo mapema mwakani lengo ni kuandaa kitu bora ambacho kitatoa fulsa kwa wengi na kuacha historia.”