Waziri Mkuu kunogesha tamasha la Wabunge Simba, Yanga

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba anatarajia kunogesha tamasha litakalowakutanisha watumishi wa Bunge na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano  wanaoshabikia klabu za Yanga na Simba akiwa mgeni rasmi.

Tamasha hilo litakaloambatana na burudani na  michuano ya michezo mbalimbali litafanyika Januari 31, 2026 jijini Dodoma.

Bonanza hilo lililoandaliwa na Ofisi ya Bunge kwa ushirikiano na Benki ya Azania, litajumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kushindana kula, kujaza maji ndani ya chupa, kukimbia na magunia netiboli, wavu na kuruka kamba.

Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Bunge, Festo Sanga akizungumza na wanahabari leo, Januari 16, 2026 amesema bonanza hilo ni maalum kwa ajili ya uzinduzi wa Bunge la 13 na Wabunge wote kwa mara ya kwanza watakutana kushiriki michezo mbalimbali.

Sanga amesema lengo la bonanza hilo ni kujenga uhusiano mwema kati ya Bunge, watumishi na taasisi
zinazofanya kazi kwa ukaribu na mhimili huo zikiwamo klabu hizo mbili kubwa nchini.

“Jambo jingine tunamuunga mkono
Rais Samia Suluhu katika kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki michezo. Ni bonanza kubwa,
tunawaomba mashabiki wa Yanga na Simba jijini Dodoma wajitokeze kwa wingi,” amesema Sanga na kuongeza;

“Lengo ni kuleta umoja na mshikamano baina ya wabunge, watumishi na taasisi mbalimbali zinazofanya kazi na bunge bonanza litanza kwa kufanya matembezi kuanzia Mipango tukimuunga mkoani Rais katika kuhamasisha wananchi ili kulinda afya.”

Sanga amesema tamasha hilo lenye kauli mbiu ya Umoja Wetu ni Nguvu Yetu, anaamini litakuwa  na ushindani mkubwa kutokana na kubeba mashabiki wa timu kongwe za Simba na Yanga ambao huwa hazina jambo dogo.

Meneja Mawasiliano Idara ya Biashara ya Benki ya Azania, Elizabeth Nyatega, amesema taasisi hiyo inajisikia fahari kuwa mshiriki wa bonanza hilo linalolenga kujenga uhusiano na kuimarisha afya.

“Jambo lolote linalowagusa wabunge, basi linawagusa wananchi. Benki yetu tunajivunia kushiriki bonanza hili na tuna morali ya hali ya juu,” amesema.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema wataendelea walipoishia baada ya mwaka jana kuwafunga watani zao Yanga msimu uliopita.

Ahmed alisema wamefanya tathimini na kubaini wabunge wengi waliochaguliwa ni Simba ukiondoa wa msimu uliopita ambao pia bado wapo nawaomba mashabiki kutoka matawi mbalimbali kutoka Dodoma kujitoleza kwa wingi.

“Matawi yote Simba mji Mkuu, Friends of Simba Dodoma na mengine mengi wajitokeze kwa wingi kuipa sapoti timu yetu ya wabunge ili tuendelee kuipa sapoti timu yetu.”

Ibrahim Samweli Mkurugenzi wa Wanachama na Masoko Yanga, amesema wanatarajia kuwakilishwa na matawi mengi waliyonayo Dodoma Jiji na wanaamini ushiriki wao utakuwa chachu ya ushereheshaji wa tamasha hilo.