Waziri wa zamani wa elimu Uganda afariki dunia

Uganda. Waziri wa Elimu wa zamani nchini Uganda, Geraldine Bitamazire amefariki dunia na akikumbukwa na mchango katika utekelezaji wa Elimu ya Msingi kwa Wote (Upe) na Elimu ya Sekondari kwa Wote (Use).

Kifo cha Bitamazire, mwenye umri wa miaka 81, kilichotokea jana Januari 15, 2026, kimethibitishwa na wanafamilia pamoja na wafanyakazi wa Taasisia ya Usimamizi ya Uganda (Umi, ambako aliwahi kuhudumu kama kansela.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Kedrace Turyagyenda amemwelezea kama nguzo muhimu ya kujitolea kwa sekta ya elimu.

“Aliitumikia sekta ya elimu katika maisha yake yote ya kazi na katika ngazi zote. Alikuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tororo na alihudumu kama Waziri wa Elimu mara tatu,” amesema Dk Turyagyenda.

“Pia alikuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa UPE [Elimu ya Msingi kwa Wote] na USE [Elimu ya Sekondari kwa Wote]. Kauli aliyokuwa akiitoa mara kwa mara ni kwamba, ‘tunataka watoto wapate elimu bora, siyo elimu tu,” ameongeza.

Profesa Barnabas Nawangwe, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Makerere, ameliambia Gazeti la Daily Monitor kuwa taarifa za kifo cha Bitamazire zilipokewa kwa huzuni.

“Geraldine Bitamazire alichangia kwa kiasi kikubwa kufufua mfumo wa elimu wa Uganda. Pia alikuwa mhimili muhimu katika kurejesha Chuo Kikuu cha Makerere baada ya misukosuko kati ya mwaka 1970 na 1980,” amesema Prof. Nawangwe.

“Amesaidia kutatua migogoro kati ya wafanyakazi wa chuo kikuu na serikali.

Tutamkumbuka kama mama na mshauri wa masuala ya elimu nchini Uganda,” ameongeza.