Moshi. Kijana Deogratius James Ottaru (37), mkazi wa Kijiji cha Kilema Kati, Kata ya Kibosho Kirima, wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, amekutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake aliyokuwa akiishi peke yake.
Taarifa zinaeleza Drogratius (marehemu) alifariki takribani siku mbili kabla ya kugundulika, hali iliyosababisha mwili wake kuvimba na kuanza kuoza, huku harufu kali ikiwashtua ndugu na majirani.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 17, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza uchunguzi unaendelea.
“Askari walipofika eneo la tukio walibaini mlango wa chumba anachoishi ulikuwa umefungwa kwa ndani. Walipoingia walikuta mwili umelala chini na kulikuwa na harufu ya pombe,” amesema Kamanda Maigwa.
Baadhi ya watu waliofika eneo la kitongoji cha Kidachini Kijiji ya Kilema Kati Kata ya Kibosho Kirima Mkoani Kilimanjaro kushuhudia tukio la Deogratius Ottaru (Marehem) kufia ndani.
Amesema kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda na majirani, marehemu alikuwa mtumiaji wa pombe kali na wakati mwingine alikunywa bila kula.
“Inawezekana ikawa ni sababu, lakini hiyo ni taarifa za awali. Mwili umechukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kwa uchunguzi ambao utaonesha chanzo halisi cha kifo,” amesema.
Mwanachi limeshuhudia askari Polisi wakifika eneo la tukio leo Jumamosi Januari 16, 2026, saa tano asubuhi, likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Moshi, wakiambatana na madaktari kwa uchunguzi.
Akizungumza katika eneo la tukio, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kidachini, Abuu Seleman Kwayi, amesema alipata taarifa za tukio hilo saa 3:30 asubuhi kutoka kwa kamanda wa sungusungu.
“Nilipofika niliwauliza wanafamilia kama walishatoa taarifa polisi, wakasema tayari walishatuma ndugu kituoni na walikuwa wakisubiri askari wafike kwa ajili ya uchunguzi,” amesema Kwayi.
Baadhi ya watu waliofika eneo la kitongoji cha Kidachini Kijiji ya Kilema Kati Kata ya Kibosho Kirima Mkoani Kilimanjaro kushuhudia tukio la Deogratius Ottaru (Marehem) kufia ndani.
Kwayi ametoa wito kwa vijana kuzingatia matumizi ya pombe na kuepuka kunywa kupita kiasi na kuishi kwa tahadhari.
“Unywaji wa pombe kupita kiasi si mzuri. Kuishi peke yako pia si salama. Kama angekuwa anaishi na mtu, huenda angepata msaada mapema,” amesema.
Ndugu wa Marehemu, Brightnes Ottaru amesema mara ya mwisho kuonana na Deogratius ilikuwa kipindi cha mwaka mpya lakini kwa hivi karibuni alishindwa baada ya juhudi za kuwasiliana naye kwa simu kugonga mwamba.
“Nilipigiwa simu leo saa tano asubuhi nikaambiwa ndugu yangu amefariki. Tulipofungua dirisha tukamwona ameanguka na amelala chini, tayari alikuwa ameshaanza kutoa harufu,” amesema.
Brightnes anasema jirani mmoja alimwambia mara ya mwisho kumuona marehemu ilikuwa Alhamisi jioni, akieleza awali aliishi na mke wake kabla ya kutengana, huku mkewe akiishi kwao lakini akimtembelea mara kwa mara.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia, mjomba wa marehemu ndiye aliyegundua tukio hilo baada ya kuona taa za nje zikiwa zimewaka asubuhi, akajaribu kugonga mlango bila majibu, kabla ya kuzunguka dirishani na kumuona Deogratius (marehemu) akiwa amelala chini na kutoa taarifa Polisi.
Rafiki wa marehemu, John Kwayi, amesema kifo hicho kimewaacha wengi katika mshtuko.
“Marehemu ni mtu niliyesoma naye darasa moja na ni jirani wa karibu. Kifo chake kimenisikitisha sana, hadi sasa siamini kama amefariki,” amesema.
Kwa upande wake, Martina Joseph Mlayi, mke wa marehemu ambaye walikuwa wametengana tangu Julai mwaka jana, amesema kuna wakati Deogratius ambaye ni marehemu alikuwa akilalamikia matatizo ya kiafya.
“Alikuwa akiniambia kuna nyakati anasikia kizunguzungu na anaanguka. Mara ya mwisho kumuona ilikuwa Alhamisi aliponitembelea nilipoishi Kwa Change,” amesema.
Martina amesema marehemu ameacha watoto watatu, wa kwanza ana miaka 14 na anatarajiwa kuanza kidato cha kwanza, wa pili ana miaka mitatu na wa mwisho ana mwaka mmoja na nusu.