CCM kuanza ziara ufutiliaji wa ahadi za siku 100

Dodoma. Zikiwa zimekaribia kutimia siku 100 tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kichukue madaraka, kwa awamu ya sita uongozi wa chama hicho umetangaza kuanza rasmi kazi ya ufuatiliaji wa ahadi za viongozi wake ikiwemo alizozitoa Rais.

Mbali na hilo, chama hicho kikongwe barani Afrika kimewataka viongozi waliomaliza muda wao kustaafu kwa heshima ili waendelee kuwa msaada ndani ya CCM na Taifa.

Hayo yameelezwa na Katibu wa itikadi Mafunzo na Uenezi wa chama hicho Kenani Kihongosi wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo Jumamosi Januari 17, 2026.

Ufuatiliaji huo unakwenda kufanyika kupita ziara za kiongozi huyo  iliyopewa jina la Kliniki ya kisiasa na itaanza Januari 19 hadi 22,2026  Mkoani Singida ambapo chama hicho kitakwenda  kukutana na wananchi kwenye maeneo hayo ili kusikiliza  kero na kuzitolea majibu.

Kihongozi amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni zinatafsiriwa kwa vitendo na kuwanufaisha wananchi katika sekta mbalimbali za maendeleo.

“Wajibu wetu ni kwenda kusikiliza umma unatuambia nini juu ya ahadi ambazo zimanzwa kutekelezwa na zile ambazo bado ila tuliahidi kuzitimiza ndani ya siku 100 hata kabla ya kutumia,” amesema Kihongosi.

Kwa mujibu wa Kihongosi, CCM ina dhamira ya dhati ya kuwajibika kwa wananchi kwa kutekeleza kwa vitendo ilani yake, akisisitiza siku 100 za mwanzo ni kipimo muhimu cha mwelekeo wa Serikali mpya katika kutimiza matarajio ya wananchi.

Kuhusu viongozi wastaafu amewaonya baadhi kufuatia kauli wanazotoa ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko ndani ya chama na Taifa kwa ujumla.

Alikuwa akijibu swali kuhusu kauli aliyoitoa Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba kufuatia kauli aliyowahi kuitoa siku za hivi karibuni alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu hali ya usalama nchini.

Katika kauli yake Jaji Warioba alinukuliwa akisema kuna mpasuko ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi ambalo alidai limemuomba alisaidie kuondoa mgawanyiko ambao umesababishwa na itikadi za kisiasa.

Kihongosi amesema “hapa niwatake viongozi wastaafu kutumika kama darasa la ushauri kwa viongozi wa sasa na si kulalamika ama kukosoa uongozi wa sasa kwa namna isiyofaa,” amesema.

“Kama chama tunamuheshimu mzee wetu Warioba tunamuomba astaafu vizuri kama wastaafu wengine na aache ulalamishi na asiwe na chuki kwa viongozi waliopo na kama anataka kutoa usharuri utaratibu upo,” amesema Kihongosi.