Dar es Salaam. Mfanyabiashara Harun Elias (26) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidaiwa kujipatia mkopo wa Sh570 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Mbali na Elias ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam mshtakiwa wa pili ni kampuni ya Javis International Trader Company Limite.
Elias na kampuni hiyo zimefikishwa mahakamani hapo jana Ijumaa, Januari 16, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 950 ya mwaka 2026 yenye mashtaka mawili, ambayo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Mshtakiwa amesomewa mashtaka hayo jana Ijumaa, Januari 16, 2026 na Wakili wa Serikali Tumain Mafuru, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.
Hata hivyo, Kabla ya kuwasomea mashtaka yao, Mwankuga aliwaeleza washtakiwa hao kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.
Vilevile kutokana shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria, mshtakiwa atapelekwa rumande.
Kisha wakili Mafuru alimsomea mashtaka yake, ambapo shtaka la kwanza ni kujipatia mkopo wa fedha njia ya udanganyifu, linalomkabili Elias na kampuni hiyo.
Inadaiwa Novemba 2017 katika Benki ya BancABC Tanzania tawi la Uhuru Height, lililopo jijini Dar es Salaam kwa njia ya uongo walipata mkopo wa Sh570 milioni kupitia akaunti namba 1711472023 yenye jina la kampuni ya biashara ya Javin International Limited kutoka African Banking Corporation Tanzania Limited (Banc ABC).
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha linalomkabili Elias na kampuni hiyo, ambapo Novemba 2017 katika Benki ya African Banking Corporation Tanzania Limited (Banc ABC) tawi la Uhuru Height, jijini Dar es salaam, washtakiwa walipata mkopo wa Sh570 milioni kutoka katika benki hiyo, huku wakijua kwamba mchakato ulitumika kupata mkopo ho ni wa kosa la tangulizi la kupata mkopo kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya kusomewa mashtaka yake, upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika.
Hakimu mwankuga aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 29, 2026 kwa kutajwa na mshtakiwa amepelekwa mahabusu gerezani.