Khambay awataka maofisa ardhi Babati kufanya kliniki ya ardhi

Babati. Mbunge wa Babati mjini, mkoani Manyara, Emmanuel Khambay amewataka maofisa ardhi wa halmashauri ya mji huo kufanya kliniki ya ardhi kwenye kata ili kuondoa migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi mbalimbali.

Khambay ametoa agizo hilo kwenye kata ya Maisaka Januari 17, 2026 katika ziara ya kushukuru kwa kuchaguliwa na kusikiliza kero, malalamiko na changamoto zinazowakabili wakazi wa eneo hilo.

Ameeleza kwamba miongoni mwa malalamiko, kero na changamoto alizozipata katika jamii ni migogoro ya ardhi kwenye Kata ya Maisaka hivyo maofisa ardhi waanzishe kliniki katika eneo hilo.

“Maofisa ardhi wa halmashauri anzisheni kliniki ya ardhi na kukutana na wakazi wa kata ya Maisaka, msikilize changamoto zao na kuwapatia majawabu,” amesema Khambay.

Ameeleza kuwa anatarajia maofisa ardhi wa halmashauri hiyo wakifanya kliniki hiyo kwa ufasaha watafanikisha kutatua migogoro hiyo ya ardhi ipasavyo.

“Lengo la ziara hii ni kuwashukuru na kusema asante kwa kunichagua na kusikiliza kero mbalimbali na miongoni mwa changamoto ni migogoro ya ardhi hivyo itatuliwe,” amesema Khambay.

Amesema tiba ya migogoro ya ardhi ni kuanzisha kliniki ya ardhi kwa maofisa ardhi kutoka ofisini na kwenda kwa watu kusikiliza matatizo yao na kueleza namna ya kuyatatua.

Hata hivyo, amewaahidi wakazi wa eneo hilo, kuendelea kushirikiana nao katika kufanikisha maendeleo na kutoa huduma bora bila upendeleo wowote ule kwa jamii.

“Nawashukuru mno kwa upendo wenu kwangu wana wa Babati mjini, naomba ushirikiano wenu katika utumishi huu uliotukuka na mlionikabidhi mimi ndugu yenu,” amesema Khambay.

Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Babati mjini, Elizabeth Malley amempongeza Khambay kwa kuchaguliwa na kushika nafasi hiyo na kujitoa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa mjini Babati.

Malley amewaomba wakazi wa Babati mjini wampe ushirikiano wa kutosha mbunge wao ili aweze kuwatumikia ipasavyo kwani uchaguzi umeshafanyika na kilichobaki hivi sasa ni kufanyika maendeleo.

Mmoja kati ya wakazi wa kata ya Maisaka, Rose John amepongeza hatua hiyo ya kufanyika kwa kliniki ya ardhi itakayofanywa na maofisa ardhi wa halmashauri hiyo.

Amesema kupitia kliniki hiyo itakayofanywa wataweza kumaliza migogoro ya ardhi ambayo kwa namna moja au nyingine inazorotesha maendeleo.