Dar es Salaam. Mkuu wa Utumishi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Marco Gaguti amefunga rasmi zoezi la ‘Medani la Ex- Maliza’ lililofanywa na Kuruti wa Kundi la 44/25 katika eneo la Msata huku akiwataka kuruti hao kuwa watiifu kwa nchi yao.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo jana Ijumaa, Januari 16, 2026, Meja Jenerali Gaguti sambamba na hilo amewataka kuruti hao wanaotarajia kuhitimu mafunzo ya awali ya kijeshi hivi karibuni kuwa waadilifu pamoja na kujituma.
Hivyo, kuruti walioshiriki zoezi, wametakiwa kuzingatia mafunzo ya nadharia na vitendo kama shambulio la kunuia, shambulio la kushtukiza na somo la doria huku akionyesha wazi kuwa zoezi limefanikiwa.
“Dhamira ya Jeshi la ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni kuona kuruti wote wanahitimu na kwenda katika maeneo mbalimbali watakayopangiwa kushiriki kulilinda taifa,” amesema.
Meja Jenerali Gaguti ameongeza mafunzo na mazoezi mbalimbali ya medani ndio msingi wa JWTZ kwani Jeshi imara linatokana na uwepo wa mazoezi ya medani.
Kuruti wanaotarajiwa kuhitimu kozi ya mafunzo ya awali wamesisitizwa kuzingatia mambo makuu manne kwa mwanajeshi ambayo ni nidhamu nzuri, uhodari, utii na uaminifu ambayo yamewajenga wanajeshi na kutekeleza majukumu kwa weledi.
Naye, Mkuu wa Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi RTS Kihangaiko, Brigedia Jenerali Sijaona Myalla amesema wanafunzi wa kozi ya mafunzo ya awali wameonyesha uwezo wa kukabiliana na adui kwa kulifanya zoezi kuwa na mafanikio makubwa.
Brigedia Jenerali Myalla amesema kuwa zoezi limewajenga kuruti kuwa na uzalendo, kudumisha mahusiano na raia, kuwajengea uwezo wa kufanya operesheni katika mazingira yoyote ndani na nje ya nchi.
“Kuruti wamejengewa ujasiri na kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika mazingira ya medani,” amesema.
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linaendelea kufanikisha kufanyika mazoezi mbalimbali ya medani kwa Kozi za Mafunzo ya Awali katika Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi RTS Kihangaiko ili kuwajengea uwezo askari wapya, namna ya kuilinda nchi ya Tanzania kwa kushirikiana na wananchi.