Mahakama yawaondoa mawakili wa Serikali kesi ya ubunge Welezo

Arusha. Mahakama Kuu Zanzibar imeamua kuwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar hawana akidi katika kesi ya kupinga uchaguzi wa Jimbo la Welezo, kutokana na kutofuata utaratibu wa kisheria wa kushiriki katika kesi hiyo.

Mahakama hiyo imefikia hatua hiyo baada ya kuridhia pingamizi lililowasilishwa na Moh’d Khamis Bussara katika maombi madogo namba 142/2025 dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Welezo na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maombi hayo yanatokana na kesi ya uchaguzi namba 30/2025 ambapo Moh’d aliwasilisha ombi la kuondolewa sharti la dhamana ya gharama katika shauri la uchaguzi linalohusu Jimbo la Welezo, ambalo bado linasubiriwa mbele ya Mahakama hiyo.

Desemba 30, 2025, wakati kesi hiyo ya uchaguzi ilipoitwa kwa ajili ya amri muhimu, Wakili wa mwombaji, Omar Said Shaaban, alipinga kujumuishwa katika akidi kwa Mawakili Wakuu wa Serikali, Said Salim Said na Mbarouk Suleiman pamoja na Wakili Mwandamizi wa Serikali Ali Issa Abdalla kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Wakili huyo alidai uwepo wa Mawakili kutoka Zanzibar katika kesi hiyo unakiuka Katiba na sheria zinazosimamia uwakilishi wa Serikali katika mashauri ya kisheria.

Jaji Haji Suleiman Khamis aliyekuwa akisikiliza pingamizi hilo alitoa uamuzi huo Januari 6, 2026 na nakala yake ikawekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama ilikubaliana kuwa kawakili hao hawana haki ya moja kwa moja ya kusikilizwa katika shauri hilo, hivyo kuwatenga rasmi katika akidi ya kesi na kuamuru kuwa uwakilishi wa walalamikiwa uendelee kufanywa na mawakili waliothibitishwa kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania.

Jaji Khamis amesema Mahakama imekubaliana kuwa uwepo wa Mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ulikuwa kinyume cha utaratibu wa kisheria, hivyo uwepo wao katika akidi ya Mahakama haukuwa sahihi na walihitaji kuondolewa kwenye mwenendo mzima wa kesi.

Awali akiwasilisha pingamizi hilo, Wakili Shaaban alidai kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania imeanzishwa chini ya Kifungu cha 59 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ikianzishwa chini ya Kifungu cha 55 cha Katiba ya Zanzibar.

Alidai kuwa ofisi hizo mbili zimeanzishwa kwa sheria mbili tofauti na zina majukumu tofauti, na kwamba mjibu maombi wa kwanza ni taasisi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayopaswa kuwakilishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania.

Alieleza Mahakama kuwa maofisa walioidhinishwa kuwakilisha pande zote mahakamani hawajumuishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Mawakili wake wa Serikali, hivyo kwa msingi huo hawapaswi kuwa akidi katika kesi hiyo kwa kukosa uwezo wa uwakilishi wa kisheria.

Wajibu maombi waliwakilishwa na Mawakili wakuu wa Serikali Allan Shija na Narindwa Sekimanga wakishirikiana na Said Salim Said, Mbarouk Suleiman Ali Issa Abdalla kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Wakili Shija alieleza kuwa anakubali Mwanasheria Mkuu wa Tanzania ndiye mamlaka sahihi ya kuwakilisha suala hilo mahakamani na kwamba katika kesi hiyo wanashirikiana na Wanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kwa mujibu wa hati iliyotolewa kwa ajili hiyo.

Wakili Said kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alidai ofisi hiyo ina masilahi makubwa katika suala hilo kwani linahusisha masilahi ya umma.

Alieleza kuwa Mbunge wa jimbo hilo alichaguliwa na wananchi wa Zanzibar, hivyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ina haki ya kuwakilisha masilahi ya umma kwa ujumla waliomchagua mwakilishi wao.

Wakili huyo alidai kuwa suala la kutoa haki ya kusikilizwa kwa Mwanasheria Mkuu katika masuala yenye masilahi ya umma si jambo jipya, huku akinukuu maamuzi mbalimbali ya mahakama kuunga mkono hoja yake.

Aliongeza kuwa Wakili wa mwombaji alishindwa kuonyesha jinsi mteja wake angeathiriwa endapo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar angeruhusiwa kuhudhuria kesi hiyo, na kusisitiza kuwa wakili wa mwombaji hapaswi kuogopa uwepo wao.

Wakili Shaaban alijibu kuwa hawakutilia shaka uwezo wa mawakili Shija na Sekimanga kwa kuwa wana mamlaka halali ya kuwakilisha wajibu maombi, na kwamba endapo kulikuwa na hati ya ushirikiano, haikuwasilishwa mahakamani.

Aliongeza kuwa iwapo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alikuwa na masilahi katika suala hilo, ilipaswa kuiarifu Mahakama na kuthibitisha kuwa suala hilo linahusu masilahi ya umma.

Jaji Khamis amesema baada ya kusikiliza hoja hizo amesema hakuna ubishi kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ni ofisi tofauti za kikatiba zilizoanzishwa chini ya Katiba tofauti na kila moja ina mamlaka yake.

Ameeleza kuwa chini ya Kifungu cha 59 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Tanzania ndiye mshauri mkuu wa kisheria wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndiye mwenye jukumu la kuiwakilisha Serikali na taasisi zake katika mashauri ya kisheria.

Vilevile, chini ya Kifungu cha 55 cha Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (Utekelezaji wa Majukumu), Nambari 6 ya 2013, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ana mamlaka ya kuishauri na kuiwakilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kisheria.

Ameeleza kuwa Msimamizi wa Uchaguzi, kwa mujibu wa Kifungu cha 20 cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa, Nambari 2 ya 2024, ni mfanyakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa, ambayo ni taasisi ya Muungano.

Kutokana na hilo, amesema uwakilishi wa wajibu maombi wote uko chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania.

Jaji ameongeza kuwa Mahakama inakubaliana kuwa vifungu vya 15(1) na (3) vya Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (Utekelezaji wa Majukumu), Nambari 6 ya 2013 ya Zanzibar, vinampa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar mamlaka ya kujitokeza katika masuala yenye masilahi ya umma.

“Hata hivyo, kifungu cha 15(4) cha Sheria hiyo kinamtaka Mwanasheria Mkuu kuiarifu Mahakama na kuiridhisha kuwa jambo husika linahusu masilahi ya umma. Kifungu hiki kinaelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa,” amesema.

Amefafanua kuwa katika kesi hiyo hakuna taarifa rasmi wala maombi yaliyowasilishwa mahakamani kuonyesha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alitaka kushiriki kwa misingi ya masilahi ya umma.

Jaji Khamis ameongeza kuwa hakuna hati yoyote iliyowapa mamlaka mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kushiriki katika kesi hiyo kwa niaba ya wajibu maombi.

Kwa kuzingatia hayo, amesema Mahakama inakubaliana na Wakili Shaaban kuwa uwepo wa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ulikuwa kinyume na utaratibu wa lazima wa kisheria.

Amehitimisha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na mawakili wake wa Serikali hawana haki ya moja kwa moja ya kusikilizwa katika shauri hilo, hivyo kuingizwa kwao katika akidi hakukuwa sahihi.

“Hivyo basi, pingamizi la awali lililowasilishwa na mleta maombi linakubaliwa, na mawakili Said, Suleiman na Abdalla kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wanaondolewa kwenye mwenendo mzima wa kesi,” amehitimisha Jaji huyo.