Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ametoa maelekezo kwa Baraza la Vijana wa Chama hicho (Bavicha) kubeba ajenda kuu za chama hicho ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Mnyika ametoa maelekezo hayo katika kikao kilichowaunganisha viongozi, makada na wafuasi wa chama hicho katika kujadili hali ya siasa nchini na tathmini ya maendeleo ya baraza hilo tangu kuasisiwa kwa chama hicho miaka 33 iliyopita.
Mambo hayo ambayo Mnyika amewataka bavicha kuyabeba na kuyatekeleza kwa ukamilifu wake ni suala la Katiba mpya, Baraza la Vijana la Taifa na kuwaunganisha vijana wote wa Tanzania kudai mabadiliko.
Leo Jumamosi Januari 17, 2026 Chadema kimefanya baraza kwa mtandao katika maadhimisho yake ya miaka 33 ya kuzaliwa kwa chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1993, ambapo pamoja na mambo mengine Mnyika amelielekeza baraza la Vijana wa chama hicho kubeba ajenda ya madai ya katiba mpya kwa uzito wa kipekee.
Katika kuonesha umuhimu wa madai hayo kwa Chadema, Katibu mkuu huyo ambaye ndiye mwasisi na kiongozi wa kwanza wa Bavicha tangu lilipoanzishwa na chama hicho mwaka 2006, amesema mahitaji yote ya vijana yakiwemo ajira, elimu bora na maji yatatokana na katiba bora itakayoweka mifumo mizuri ya uongozi.
“Pamoja na mambo mengine yote tunayopigania kwa sasa, Bavicha ibebeni kwa uzito mkubwa sana sxafariya madai ya katiba mpya, najua wapo watakaowakatisha tamaa kwa mambo haya na yale lakini simamieni ajenda hii kwa nguvu zote.
“Mahitaji mengine yote kama ajira, maji, elimu bora yatapatikana ikiwa taifa litakuwa na mifumo bora ya uongozi utakaotokana na katiba bora,” amesema Mnyika, akisisitiza kuwa matatizo mengi yanayolikabili Taifa kwa sasa ni matokeo ya mifumo mibovu ya uongozi inayojengwa na katiba mbovu.
Mbali na katiba mpya, Mnyika amewapa vijana hao jukumu la kuchochea ajenda ya kuanzishwa kwa baraza la vijana la Taifa, akisisitiza ndio msingi mkubwa uliopelekea kuanzishwa kwa Bavicha.
“Kuanzishwa kwa Taifa kulilenga kuchochea upatikanaji wa Baraza la Taaifa la vijana, ambalo tangi mwaka 1998 niliingia kwenye asasi za kiraia za masuala ya vijana nilikuta ajendahiyo ikiendelea kwa msukumo mkubwa.
“Vijana wa Bavicha mnalo jukumu kuchochea uanzioshwaji wa baraza hili ili kuwapa sauti vijana fursa ya kushiriki kikamilifu katika masuala yanayowahusu na mustakhabali wa nchi kwa ujumla,” amesema.
Mnyika pia, amewaelekeza Bavicha kuwa sauti ya vijana nchini katika kupaza sauti za mahitaji na mawazo yao kwa serikali na vyombo mbalimbali vya maamzi ili kusaidia juhudi za kutatua changamoto zinazowakabili vijana nchini.
“Kuweni sauti ya vijana wa Tanzania katika kuibua hoja na kusemea mahitaji yao mkitumia fursa mliyonayo ya teknolojia na ubunfu kuwaunganisha vijana na kufikisha taarifa panapohusika,” amesema.
Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Mnyika amewatoa hofu vijana hao katika safari ya kudai mabadiliko ya mifumo ya kisiasa kuwa Chama hicho kinaaminiwa na watu wengi hivyo kitafikia malengo yake kirahisi.
Amesema licha ya changamoto za kimifumo na vitisho vya kiusalama vinavyoendelea kwa wafuasi wa vyama vya siasa zikiwemo mkesi za kisiasa kw viongozi na chama, fursa ya uungwaji mkono na wananchoi wengi ni mtaji wanaotakiwa kuutumia vijana hao kupata nguvu ya kutafuta mabadiliko hayo.
Akizungumza katika kongamano hilo kwa njia ya mtandao, Mwenyekiti wa Bavicha, Deogratius Mahinyila, ameahidi kuyabeba majukumu hayo ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini kama yalivyotolewa na Katibu wake Mkuu wa Chama.
Mahunyila amesema vijana wa Baraza hilo wataendelea kuwa mstari wa mbele katika kusukuma ajenda za chama hicho ikiwemo madai ya katiba mpya huku akisisitiza vijana wanaojiunga siasa za upinzani hawaingii wakitarajia kukumbana na vitisho vya kiusalama wanavyokumbana navyo katika shughuli zao akiwataka vijana kutokata tamaa.
“Tumesikia maelezo yako mazuri ufafanuzi kuhusu mkwamo wa baraza la vijana ambao upo katika kanuni, sisi vijana tutalibeba jukumu hili tutaendelea kupaza sauti zetu kuhakikisha tunafikia malengo hayo,” amesema.
Mahinyila amesema Bavicha wataendelea kushikilia msingi wa kigezo cha umri wa chini ya miaka 35 kwa vijana wanaogombea uongozi wa baraza hilo ili kulinda nafasi yake kuwa chombo kinachoongozwana vijana badala ya kuangukia kwa watu wazima ambao wanaweza kuacha ajenda za msingi za vijana.
“Kuhusu umri wa kugombea uongozi tutaendelea kuzingatia kuwa wanaopata nafasi ya kuliongoza baraza hili wanabaki kuwa vijana, hiindiyo tofauti ya bavichana mabaraza ya vyama vingine,” amesema.