Mrithi wa Camara huyu hapa

UNAWEZA kusema zama za Moussa Camara ndani ya Simba zimefika mwisho, hii ni baada ya uongozi wa timu hiyo kufanikiwa kumnasa kipa Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo, raia wa Niger kutoka Association Sportive des Forces Armées Nigériennes (AS FAN) iliyopo Niamey nchini humo ambayo inamilikiwa na jeshi la nchi hiyo.

Usajili wa kipa huyo umeulazimu uongozi wa Simba kumtoa kwenye mfumo kipa namba moja wa kikosi hicho, Moussa Camara ili kupunguza idadi ya nyota wa kigeni, lakini pia kufuata kanuni ambayo inaruhusu timu za ligi kusajili kipa mmoja wa kigeni.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa wamefikia uamuzi wa kusajili kipa wa kigeni kutokana na muda wa Camara anaotakiwa kukaa nje akiuguza jeraha lake la goti huku wakiwa na mechi ngumu za kimataifa mbele yao.

“Ni kweli umefanyika usajili wa kipa wa kigeni ambaye mapema wiki ijayo atawasili nchini kukamilisha mchakato lakini pia kuanza majukumu yake haraka kwani kocha amehitaji kipa wa kusaidiana na Hussein Abel.

“Haukuwa mchakato rahisi kwani tulihitaji kipa wa daraja la juu, hivyo jopo liliundwa kwa kusaidiana na kocha, tunashukuru hili limefanikiwa na tunaamini atakuwa kipa bora akiipambania Simba kufikia malengo,” kimeeleza chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema wamefanya chaguo sahihi kwa wakati sahihi wakiamini lango lao sasa litakuwa imara chini ya kipa huyo ambaye wamemtaja kuwa amekuja kutengeneza ufalme wake Ligi Kuu Bara kama ilivyokuwa kwa Camara.

Kipa huyo alikuwa namba moja kwenye kikosi cha Niger kilichoshiriki Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) zilizofanyika mwaka 2025 nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

Katika mechi ya Kundi C dhidi ya Afrika Kusini iliyomalizika kwa timu hizo kushindwa kufungana, kipa huyo aliibuka na tuzo ya mchezaji bora.

Wakati mchakato huo ukienda vizuri na viongozi wa timu hiyo kufurahia, inaelezwa kuwa Camara ambaye alianza mazoezi ya kujiweka tayari akikaribia kurudi rasmi uwanjani, ameomba kulipwa fedha yake ya mkataba wa miezi sita uliobaki ili aende akajipambanie na sio kutolewa kwenye mfumo kusubiri hadi mwisho wa msimu mkataba umalizike.

“Licha ya kukamilisha mchakato wa kumnasa kipa huyo, kuna kazi ya kufanya kuhakikisha tunamalizana na Camara vizuri kwani hakutarajia kama tutafanya usajili wa mrithi wake, aliamini tutamsubiri hadi atakapokuwa sawa.

“Haijawa rahisi kufikia makubaliano ya kumtoa kwenye mfumo wa usajili zaidi ametaka alipwe fedha yake ya mkataba uliobaki ili akatafute nafasi nyingine nje ya Tanzania kwani haoni nafasi yake tena ya kurudishwa ndani ya Simba,” kimefichua chanzo hicho.

Camara ambaye alitua Simba msimu uliopita akitokea Horoya AC ya kwao Guinea, alisaini mkataba wa miaka miwili unaofikia tamati Juni 2026, hivyo umebaki muda wa miezi sita.

Ndani ya Simba, Camara kabla ya kuumia amekuwa kipa namba moja ambapo msimu wa kwanza amemaliza kinara wa clean sheet Ligi Kuu Bara akiwa nazo 19 akicheza mechi 28, huku akiifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2024-2025.

Kinachomtokea Camara sasa ni sawa na Ayoub Lakred ambaye pia aliitumikia Simba kwa msimu mmoja na kuisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo msimu wa 2023/24, aliondolewa kwenye mfumo kutokana na kusumbuliwa na majeraha aliyoyapata kwenye maandalizi ya msimu 2024-2025. Alipoondolewa Ayoub, ndipo akasajiliwa Camara.

Kama ambavyo Mwanaspoti lilikuhabarisha hapo awali, jana mchana Simba ilimtambulisha rasmi winga mpya kutoka Senegal, Libasse Gueye mwenye umri wa miaka 22 kutoka FC Teungueth ya nchini humo.

Winga huyo mwenye uwezo wa kucheza kulia na kushoto, pia anacheza kiungo mshambuliaji wa kati ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili hadi Desemba 31, 2028.

Huu ni utambulisho wa kwanza kwa Simba katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa Januari 1, 2026 na kutarajiwa kufungwa Januari 30, 2026.