Dar es Salaam. Tume ya Uchaguzi Uganda (EC) imemtangaza Yoweri Museveni kuwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu akipata asilimia 71.6 ya jumla ya kura halali zilizopigwa na kuendeleza utawala wake zaidi ya miongo minne.
Mpinzani wake Mkuu, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine alipata asilimia 24.72 ya kura zote zilizopigwa.
Bobi Wine ambaye amedaiwa kukimbia nyumbani kwake baada ya polisi kuvamia juzi, alikataa matokeo hayo ya uchaguzi akidai kuwa ni ya uongo.
Upinzani umepinga uhalali wa mchakato mzima wa uchaguzi huo, ambapo watu takribani 10 walilipotiwa kufariki dunia baada ya kuvamia kituo cha polisi eneo la Butambala kutokana na maaskari kujihami kwa kuwafyatulia risasi.
Vurugu hizo ziliripotiwa jana Ijumaa katika eneo la Butambala, kilomita 55 kusini-magharibi mwa Kampala, polisi walisema wafuasi wa Bobi Wine waliokuwa na silaha za jadi zikiwemo mapanga walijaribu kuvamia kituo cha polisi na kituo cha kuhesabia kura, hali iliyolazimu askari kufyatua risasi kujilinda na kuwakamata watu 25.
Msemaji wa Polisi Butambala, Lydia Tumushabe amesema, “Tukio hilo lilihusisha wahuni wa NUP waliokusudia kuchoma mali ya umma na waliokamatwa watafunguliwa mashtaka ya uharibifu wa makusudi.”
Taarifa hiyo ya Polisi imepingwa na Mbunge wa NUP kutoka Butambala, Muwanga Kivumbi, ambaye ameripoti kuwa vikosi vya usalama vilivamia nyumba yake baada ya upigaji kura kukamilika na kuwaua watu kumi waliokuwa eneo hilo.
Mke wake, Zahara Nampewo, ambaye ni mwanasheria mbobevu, amesema waliouawa walikuwa mawakala wa vituo vya kuhesabia kura wa NUP waliokuwa wamejificha kwenye gereji na kwamba miili yao iliondolewa na vikosi vya usalama.
Mvutano huo umeongezeka zaidi baada ya Bobi Wine mwenyewe kuripoti kuwa ameyakimbia makazi yake kufuatia vikosi vya usalama kuvamia nyumbani kwake na kuiweka chini ya ulinzi mkali familia yake.
Bobi Wine ambaye ni mpinzani mkuu wa Rais Museveni amesema kuwa polisi na jeshi walizingira makazi yake tangu Ijumaa usiku, na kwamba alifanikiwa kutoroka kabla hawajazingira eneo hilo huku mke wake na familia wakiachwa chini ya ulinzi mkali.
Chama chake cha NUP kimeripoti makazi ya kiongozi wao, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine yamezingirwa na vikosi vya usalama, hatua waliyoitaja kama kifungo cha nyumbani.
Hatua hiyo Polisi wa Uganda wameikanusha wakisema kinachofanyika nyumbani kwa mwanasiasa huyo wa hajawekwa chini ya kifungo cha nyumbani au kutekwa, wakisema uwepo wa askari ni sababu za kiusalama kwa mgombea huyo wa urais.
Mvutano baina ya Bobi Wine na vyombo vya usalama ulianza tangu wakati wa kampeni na sasa umezidi kuchukua sura mpya kadiri mchakato wa uchaguzi ulipozidi kusogea kumpata mshindi wa urais wa Taifa hilo la Afrika Mashariki.
Hali ya utulivu nchini humo imebadilika tangu Tume ilipoanza kutangaza matokeo ya awali jana Ijumaa ambayo yalimeendelea kumpa ushindi Rais wa sasa Yoweri Museveni, hasa baada ya kuhesabiwa takribani asilimia 60 ya vituo vya kupigia kura, Museveni akiongoza kwa asilimia 75.4 ya kura dhidi ya asilimia 20.7 za Bobi Wine wa Chama cha National Unity Platform (NUP).
Tume hiyo hata kabla ya kutangaza matokeo ya mwisho leo Jumamosi Januari 17, 2026, mwelekeo wa matokeo tangu awali ulikuwa ukionyesha Museveni, nafasi ya kuanza muhula wake wa saba.
Ushindi wa Rais Museveni umefunikwa na hali ya sintofahamu, madai ya ukandamizaji na vurugu za baada ya uchaguzi, ambapo kwa baaadhi ya maeneo hasa kusini magharibi mwa jiji la Kampala vifo kadhaa vimeripotiwa.
Kufuatia sintofahamu hiyo ambayo imeibuka nchini humo katika mazingira ambayo intaneti na huduma ya mawasiliano ya kimtandao imezimwsa tangu kuanza kwa uchaguzi huo.
Polisi nchini humo wamesema takribani watu kumi wameuawa katika matukio yaliyotokea katikati mwa nchi hiyo wakidai vifo hivyo vilitokana na makabiliano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani.
Uchaguzi huo pia ulifanyika katika mazingira ya kuzimwa mtandao wa intaneti nchi nzima umeongeza ukosolewaji kutoka upinzani na makundi ya haki za binadamu, ikiwemo
Katika taarifa yake, UN ilikosoa uchaguzi huo ikisema umefanyika katika mazingira ya ukandamizaji na vitisho kauli inayoongeza mashaka kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini humo kufuatia uchaguzi huu uliokuwa na ushindani mkali.