Mwanza. Taka 420,000 za plastiki zikiwemo nyavu za uvuvi zilizotelekezwa katika fukwe za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa sawa na asilimia 74 za taka hizo zimekusanywa katika maziwa hayo hali inayohatarisha maisha ya viumbe wa majini pamoja na uchafuzi wa maziwa hayo.
Utafiti uliofanyika katika fukwe 48 za Ziwa Victoria, tisa za Ziwa Tanganyika na 12 za Ziwa Nyasa kupitia mradi wa Clean Shores Great Lakes uliotekelezwa 2022 umeonesha pia asilimia 11 ya taka hizo zilikuwa vipande vya nguo, huku chupa na mifuko ya plastiki zikichangia karibu asilimia 40 ya taka zote.
Matokeo hayo yameelezwa Januari 16, 2026 na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bahati Mayoma wakati akiwasilisha athari za nyavu zilizotelekezwa katika kikao cha kutambulisha mradi wa kusafisha fukwe na kuondoa nyavu zilizotelekezwa katika Ziwa Victoria.
Nyavu zikiwa zimehifadhiwa kwenye boti katika Kisiwa cha Bezi Wilaya ya Ilemela mkoani. Picha na Saada Amir
Dk Mayoma amesema asilimia 90 za nyavu zilizobainika na zinazotumika na wavuvi kuvulia samaki zimetengenezwa kwa plastiki.
“Mwaka 2014 tulifanya utafiti ambao ulikuwa umetanguliwa na tafsiri ambao walikuwa wameshafanya utafiti kuhusu hali ya taka ngumu kwenye maji mafupi na hao wenzetu waligundua mwaka 2013 kwamba kulikuwa na nyavu nyingi sana ambazo zinaelea katika maji mafupi,
“Takwimu zilionesha zile nyavu za makila zilikuwa asilimia 44 na zile nyavu zinazokubalika kisheria zilikuwa asilimia 42. Nawahakikishieni tatizo la nyavu pamoja na nguo lipo zaidi katika kina kifupi,” amesema Dk Mayoma.
“Vipande vingi tulivyovikuta ni vile vilivyo katika muundo wa nyuzi nyuzi … sasa huwezi kukuta nyuzi imetoka kwenye chupa ya plastiki . Plastiki ikivunjika kinakuwa kipande cha duara au cha mviringo … kama ni nyuzi imetoka kwenye nguo au kwenye nyavu,” amesema.
Akizungumzia chanzo cha tatizo hilo, Mwenyekiti wa Beach Management Unit (BMU) Wilaya ya Nyamagana, Joel Mshola, amesema wavuvi wengi hukata nyavu zilizoharibika na kuzitupa ziwani, hali inayosababisha nyavu hizo kuendelea kujikusanya majini na kusombwa hadi fukwe.
“Magugu maji pia husomba nyavu hizi na kuzifanya ziwe chanzo kikubwa cha uchafuzi wa fukwe,” amesema.
Wavuvi wa kisiwa cha Bezi Wilayani Ilemela wakitengeneza nyavu kwaajili ya uvuvi. Picha na Saada Amir.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uhifadhi Mazingira ya Mto Mirongo jijini Mwanza, Adam Shija ameshauri BMU kutunga sheria ndogo na kuanzisha maeneo maalumu ya kukusanyia taka katika mialo.
“Taka nyingi zinaishia kwenye fukwe kwa sababu jamii haina uwezo wa kufanya urejeshaji. BMU zikianzisha collection points, tatizo linaweza kudhibitiwa,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa BMU Igombe wilayani Ilemela, Thadeo Philipo amesema idara ya uvuvi inapaswa kuwezeshwa ili iweze kudhibiti uingizaji na matumizi ya nyavu haramu zinazochangia uchafuzi wa mazingira.
“Hakuna uchafu unaoharibu ziwa kama nyavu za timba. Fisheries wawezeshwe vifaa na watu ili waweze kufanya misako na kuchukua hatua,” amesema.
Mmiliki wa mitumbwi, Majula Masoko amesema changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu ya uhifadhi kwa wavuvi, na kuitaka Serikali kuongeza juhudi za kutoa elimu moja kwa moja katika maeneo ya uvuvi.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, Shirika la Blue Victoria limeanzisha mradi wa kuzuia utelekezwaji wa nyavu Ziwa Victoria (Stop Fishing Ghost Gears) utakaotekelezwa kuanzia Januari 18 hadi 28, 2026 katika fukwe 10 za wilaya za Ilemela na Nyamagana.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Festus Massaho amesema mradi huo unalenga kupunguza uchafuzi wa ziwa na upotevu wa viumbe hai kupitia ukusanyaji wa nyavu zilizotelekezwa na ufuatiliaji wa mialo.
Akitoa mapendekezo ya suluhisho la muda mrefu, Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (Saut), Dk Nesmo Kaganga, amesema viwanda na wabunifu wanapaswa kushirikishwa ili kubuni bidhaa zitakazotumia nyavu zilizoisha matumizi kama malighafi.
“Kwa kufanya hivyo, tutapunguza taka, kuokoa mazingira na kuongeza thamani ya kiuchumi,” amesema.