OUT yachunguza madai ya udanganyifu wahitimu wa 2025

Dodoma. Uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) umekiri kupokea taarifa zinazodai uwepo wa udanganyifu kwenye  matokeo ya wahitimu wa chuo hicho wa mwaka 2025, kufuatia mjadala uliozuka hivi karibu.

Kauli hiyo inakuja kufuatia taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa, zikidai uwepo wa udanganyifu kwenye matokeo ya wahitimu zaidi ya 300 wa chuo hicho, waliohitimu Novemba mwaka jana.

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano kwa OUT, Dk Adam Namamba amesema uchunguzi ukikamilika na kubainika kuhusu jambo hilo, hatua kali zitachukuliwa na hakuna atakayekuwa juu ya sheria.

Kwa muhibu wa madai hayo, baadhi ya wahitimu, wengi wao walikuwa watumishi wa umma kutoka sekta nyeti za Serikali, walighushi matokeo yaliyowawezesha kupata vyeti vya kuhitimu taaluma zao kwa njia isiyo halali.

Taarifa hizo zimeeleza namna mpango huo ulivyosukwa lengo likiwa kuwasaidia baadhi ya watumishi kupata vyeti vya kitaaluma kwa ngazi mbalimbali.

“Kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uadilifu wa kitaaluma na kulinda imani ya wadau wa elimu, chuo kimeanzisha mchakato wa tathmini na uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini uhalisia wa taarifa hizo,” anasema Dk Namamba.

Amesema mchakato huo unatekelezwa kwa kushirikiana na mamlaka husika za ndani ya chuo na taasisi zingine zinazohusika kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi.

Hata hivyo, taarifa hiyo pia imeeleza kuwa, baadhi ya takwimu na maelezo yaliyotolewa kupitia taarifa zilizosambaa kwenye  mitandao kuhusu ukubwa wa tukio hilo, zinakinzana na taarifa za awali zilizopo, hivyo zinahitaji uthibitisho zaidi kupitia mchakato unaoendelea.

Kadhalika Dk Namamba amesema mara baada ya uchunguzi huo kukamilika na ikabainika uwepo wa wahusika wa tukio hilo, chuo hakitasita kuwachukulia hatua stahiki kwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi na taratibu za kitaaluma.

Uongozi huo pia umeahidi kuwa chuo hicho kitaendelea kusimamia viwango vya juu vya ubora wa kitaaluma, uwajibikaji na uadilifu kama ilivyo azma yake na misingi ya uanzishwaji wake.