Pogba wa Zenji aibukia KMC

KIUNGO mshambuliaji wa Mlandege, Juma Kidawa ‘Pogba’ aliyekuwa akihusishwa kutua Azam FC, ameibukia KMC kwa kusainishwa mkataba wa miaka ili kuitumikia timu hiyo inayopambana kujiweka katika nafasi nzuri kutokana na kuanza vibaya msimu.

Pogba ambaye mwanzoni mwa msimu alikuwa akihusishwa kutua Simba kabla ya mpango wake kufa baada ya wekundu hao kumnasa Daud Semfuko kutoka Coastal Union tayari amevuka maji na kusaini mkataba huo muda wowote kuanzia sasa ataanza mazoezi na timu hiyo.

Chanzo cha kuaminika kutoka Mlandege kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli wamefanya biashara na KMC ya kumuuza kiungo huyo ambaye alikuwa na ofa nyingi kutoka bara dirisha hili la usajili.

“Tunamtakia kila la heri na tuna imani kubwa kwamba ataenda kufanya mambo makubwa ndani ya KMC kutokana na kipaji alichonacho ameahidi kuwa bora na kuipeperusha vyema Mlandege Ligi kuu Bara.”

Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta mchezaji huyo ambaye alikiri kuwa anatua kucheza Ligi Kuu Bara, lakini hayupo tayari kuweka wazi ni timu gani kwa sababu hiyo sio kazi yake.

“Mimi kazi yangu ni kucheza na ni kweli nimesaini moja ya timu, lakini yenyewe ndio ina nafasi kubwa ya kutoa taarifa sio mimi. Mkataba wangu unanizuia kuizungumzia timu bila  kupewa ruhusa ya kufanya hivyo,” alisema mchezaji huyo akifananishwa kiuchezaji na Paul Pogba aliyepo Monaco ya Ufaransa kwa sasa akiwahi kuzitumikia pia Manchester United na Juventus.

“Nawa shukuru viongozi wa Mlandege kwa kuniamini muda wote tuliokuwa pamoja na kunipa nafasi ya kuja kujaribu changamoto mpya Bara.

“Nimekuja kupambana na kuiheshimisha timu hiyo, naamini ushirikiano mzuri baina yangu uongozi na wachezaji ndio kitu kimenifikisha hapa.”

KMC inayonolewa na kocha wa zamani wa Mlandege, Abdallah Mohammed ‘Baresi’ ndio inayoburuza mkia kwa sasa katika Ligi Kuu Bara ikicheza mechi tisa na kuvuna pointi nne katika michuano hiyo, ikishinda mechi ya awali dhidi ya Dodoma Jiji na kutoka sare na Mtibwa Sugar ikipoteza nyingine saba.