Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema matamanio yake ni kuona vijana wanawekeza zaidi katika mfuko wa faida.
Mfuko huo ambao ni mpango wa wazi unaotoa fursa ya uwekezaji kwa Watazania hasa wa kipato cha kati na chini kupitia uwekezaji katika vipande ili kupata mapato shindani kupitia ukuaji wa mitaji; na kutengeneza utamaduni wa kuwekeza katika Masoko ya Fedha na Mitaji.
Mfuko huo unaoujumuisha wawekezaji wa kada zote kuanzia wawekezaji wadogo kama vile bodaboda, wanafunzi, wafanyakazi, wastaafu, wakulima hadi wawekezaji wakubwa.
Akizungumza leo Jumamosi Januari 17, 2025 kwenye mkutano mkuu wa tatu wa mwaka wa uwekezaji wa mfuko wa FAIDA FUND ulioandaliwa na Watumishi Housing Investments (WHI) amesema uhamasishaji hasa kwa vijana ni jambo bora na lisilo epukika.
Ridhiwani amesema kuna vijana wengi kutoka sekta mbalimbali walio fanikiwa ambao wanahitaji kuelekezwa juu ya njia zilizo bora na salaama katika uwekezaji.
Amesema vijana hao pamoja na wafanyabiashara wakipata elimu ya uwekezaji watawekeza zaidi kwenye mfuko huo ambao ni akiba na wenye thamani.
“Kwa mujibu wa taarifa ya usimamizi wa mfuko hadi Juni mwaka 2025, ukubwa wa mfuko uliongozeka hadi Sh43.9 kutoka Sh25 bilioni kwa mwaka uliopita ikiwa na ongezeko la Sh18 bilioni,” amebainisha.
Ridhiwani amesema kwa sasa kuna kampuni zaidi ya 200 zimewekeza huku wawekezaji wakiongezeka:”Menejimenti iendelee kukutana na taasisi mbalimbali ili Watanzania na kampuni zote ziwe sehemu ya wadau wakubwa wa mfuko huu.”
“Kuna watumishi wa Serikali 1200 wamewekeza idadi hii kwangu ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watumishi wote wa umma, natumia fursa hii kuwahimiza kuchangamkia fursa hii ili kujiwekea akiba, uhuru wa kifedha na katika kujiandaa kustafu,” amesema.
Ametaka menejimenti hiyo kujitanganza na kutoa elimu kwa umma ili Watanzania wachangamkie fursa huyo.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi WHI, Fortunatus Magambo amesema mfuko huo kwa sasa unazidi kukua ikiwa ni hatua yenye tija kwa maendeleo.
Amesema kwa sasa una wawekezaji 12000 kutoka 8000 wakiemoi vijana huku akisema elimu zaidi ya uwekezaji inatolewa kuongeza wawekezaji zaidi kama alivyosema Waziri.
Amesema elimu ya fedha inatolewa na itazidi kutolewa hasa katika uwekezaji ili kupata wawekezaji wengi zaidi.