Taasisi ya Rotaract Club of Young Professionals Tanzania leo imetoa msaada wa viti na meza za kusomea pamoja na kichomea taka kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Toa Ngoma, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia shuleni hapo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, mwakilishi wa taasisi hiyo Glory Mwankenja amesema msaada huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.5 za Kitanzania unalenga kuwasaidia wanafunzi kwa ujumla, hususan wale wenye changamoto za uoni, ili waweze kusoma katika mazingira salama, rafiki na yenye motisha.
Mwankenja ameongeza kuwa Rotaract inaamini elimu bora huanzia na mazingira bora, hivyo wameamua kushirikiana na jamii kusaidia shule zinazokabiliwa na changamoto za miundombinu na vifaa vya msingi vya kujifunzia.
Aidha, uongozi wa shule hiyo umeushukuru uongozi wa Rotaract kwa msaada huo, wakisema utapunguza uhaba wa samani darasani na kuongeza usafi wa mazingira kwa kuwepo kwa kichomea taka, jambo litakalosaidia kulinda afya za wanafunzi.
Rotaract ni jumuiya ya vijana wataalamu inayofanya kazi chini ya mwamvuli wa Rotary International, ikilenga kuwajenga vijana kupitia huduma kwa jamii, uongozi na maendeleo ya taaluma.
Nchini Tanzania, Rotaract Club of Young Professionals Tanzania imekuwa mstari wa mbele kushiriki katika miradi ya kijamii kama elimu, afya, mazingira na uwezeshaji wa vijana, kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kukuza uzalendo wa kushiriki maendeleo.
Kupitia miradi kama huu wa Shule ya Msingi Toa Ngoma, Rotaract inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuunganisha taaluma na huduma kwa jamii kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.



