Straika apewa miwili Fountain | Mwanaspoti

FOUTAIN Gate imekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship, Boniface Mwanjonde baada ya kuonyesha kiwango bora msimu huu.

Mchezaji huyo alikuwa akifuatiliwa mara kwa mara na Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’ ambapo tayari amekamilisha usajili, huku mabosi wa kikosi hicho wakimpa mkataba wa miaka miwili.

Mshambuliaji huyo amehusika na mabao 13 katika mechi 14 alizoichezea Mbeya Kwanza baada ya kufunga tisa na kuasisti manne, huku akiwa miongoni wa wachezaji wawili waliofunga mabao matatu katika mechi (hat-trick) za Championship sawa na Mzambia Obrey Chirwa wa Kagera Sugar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer alisema lengo la timu hiyo ni kuendelea kuboresha maeneo mbalimbali katika dirisha hili dogo la usajili ili kuendana na ushindani uliopo msimu huu.

“Ripoti yangu kwa uongozi niliiwasilisha mapema kwa sababu miongoni mwa maeneo ninayohitaji yaongezewe nguvu ni eneo la ushambuliaji. Siwezi kusema ni mchezaji gani tunayemhitaji, ila mashabiki watajionea wenyewe,” alisema.

Fountain ilikuwa inatafuta mshambuliaji wa kuongeza nguvu baada ya kucheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara msimu huu, huku safu ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao manne na kuruhusu nyavu kutikiswa mara 12.

Timu hiyo ya Fountain inatarajiwa kushuka uwanjani Jumanne ijayo jijini Dar es Salaam kuvaana na Azam FC katika mechi itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex kabla ya saa 1:00 usiku Singida Black Stars kucheza na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa KMC Complex.