Moshi. Mamia ya vijana waliojiita ‘Genz’ ambao wamesababisha kiongozi wa dini kuondoka katikati ya ibada ya mazishi ya kijana Michael Rambau (21) kwa kufanya vurugu wamefanya mazishi wenyewe huku wakimtaka ‘DJ’ kuwawekea wimbo wa ‘Kamanda’ maarufu ulale pepa peponi Kamanda.
Ibada ya maziko ya kijana huyo ambaye ni dereva bodaboda na fundi bomba imevurugika leo Januari 17 baada ya mamia ya vijana hao ambao ni dereva bodaboda kumvamia kiongozi wa dini aliyekuwa akiongoza ibada hiyo, wakishinikiza kuambiwa ukweli juu ya kifo chake.
Kijana huyo ambaye ni fundi bomba na dereva bodaboda mkazi wa mtaa wa Karikacha, kata ya Rau, Mkoani Kilimanjaro anadaiwa kujinyonga kwa kutumia mkanda akiwa mahabusu alikokuwa akishikiliwa Januari 13, 2026 kwa tuhuma za kumjeruhi baba mdogo wake kwa kumpiga bapa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 14, 2016 na Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, mtuhumiwa huyo alikuwa akituhumiwa kufanya tukio la mauaji ya baba yake mzazi Novemba 22, 2025 kwa kumchoma na kitu chenye ncha Kali shingoni na kutoroka hadi alipokamatwa Januari 13, kwa kosa la kumshambulia na kumdhuru baba yake mdogo, Brian Felix.
Hata hivyo, baada ya kuondoka kwa kiongozi huyo wa dini, kiongozi wa Maderava bodaboda aliyejitambulisha kama ‘Genz’ alichukua kipaza sauti kwa mshereheshaji (MC) na kuwataka waombolezaji waliokuwepo katika mazishi hayo kusikiliza maelekezo aliyokuwa akiyatoa.
Vijana wakiwa wamelizingira jeneza lenye mwili wa Michael Rambau leo Jumamosi Januari 17, 2026 nyumbani kwao Moshi, Kilimanjaro.
Muda mfupi baadaye, aliwataka waombolezaji waliokuwa kwenye mazishi hayo kuanza shughuli ya kuaga mwili wa dereva bodaboda mwenzao na baada ya kumalizika aliwataka madereva bajaji na bodaboda kuwasha pikipiki zao wakati mwili ukiingizwa kaburini kama sehemu ya heshima ya kumuaga mwenzao.
Wakati mwili huo ukiingizwa kaburini na pikipiki zikinguruma alimtaka DJ kupiga wimbo wa ‘Kamanda’ huku akitoa sharti la kutokupiga picha wala video katika mazishi hayo.
Baada ya kumalizika kwa shughuli hiyo watu walitawanyika na kuondoka eneo la mazishi wengine wakitembea huku wengine wakikimbia wakihofia vurugu za vijana hao wa bodaboda wakiacha taratibu za maziko zikimaliziwa.
Alichokisema Padri wakati wa mahubiri.
Awali, akihubiri katika ibada hiyo, Padri Joseph Ndeonasia wa Parokia teule ya Mt. Stephano Shahidi- Kariwa, amewataka vijana kuishi maisha mema ya kumkumbuka Mungu kabla hazijaja siku zilizo mbaya ambapo watashindwa kusema.
“Vijana tumkumbeke sana Mungu siku za ujana wetu kabla hazijaja zile siku zilizo mbaya. Tukumbuke mwenyezi Mungu na tufahamu kabisa imani ndiyo kitu kinaenda na wewe tangu mwanzo mpaka mwisho wa maisha yako,” amesema Padri huyo.
Waombolezaji wakiwa katika msiba wa kijana Michael Rambau anayedaiwa kujinyonga mahabusu.
“Tutambue uhai ni wa nwenyezi Mungu na tumuheshimu Mungu aliyetupa uhai huku tukitambua kuwa sisi ni marehemu tunaotembea na muda wowote tunaweza tukaondoka.”
Amesema katika maisha ya hapa duniani kila mmoja anapaswa kumheshimu Mungu na kuyaishi maisha yanayompendeza ili kuwa na mwisho mwema.
“Ndugu zangu vijana, tuyaishi maisha yanayompendeza Mungu na Tufuate taratibu zote tunavyoelekezwa na kanisa, wazazi na hata jumuiya, tuwasikilize wote wanaotushauri mashauri ambayo yanampendeza Mungu,” amesema Padre huyo.
Amesema:”Tunapokuwa Hai tushauriane vizuri na katika vikundi vya umoja kama wafanyabiashara, bodaboda na wengine tushauriane vizuri. Na katika umoja huo upambwe na tunu njema, kama upendo, amani na utulivu. Tuilinde imani yetu.”
Ilivyosomwa historia ya marehemu
Akisoma historia ya marehemu, Livinus Mushi, amesema marehemu alizaliwa Mei 9, 2004 katika mtaa wa Karikacha, kata ya Rau akiwa ni mtoto wa pili katika familia ya Rambau.
“Ndugu Michael Rambau alisoma na kuhitimu elimu yake ya msingi mwaka 2017 na alisoma shule ya Sekondari Rau na baadaye alijiunga na masomo ya ufundi stadi (Veta) na kupata mafunzo ya ufundi bomba,” amesema.
Akieleza sababu ya kifo cha kijana huyo: “Mpendwa wetu Michael Rambau alifikwa na umauti akiwa mahabusu Januari 13, 2026.”
Hata hivyo, mara baada ya kueleza sababu za kifo mamia ya vijana hao walianza kulete vurugu wakitaka kujua alikufaje akiwa mahabusu jambo ambalo hakuna aliyeweza kulipatia majibu.