Wafanyakazi kortini wakidaiwa kumuibia mwajiri wao Sh1.478 bilioni

Dar es Salaam. Wafanyakazi tisa wa kampuni ya Vita Foam (T) Limited, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwana mashtaka ya wizi wa Sh1.478bilioni pamoja na kutakatisha kiasi hicho cha fedha, mali ya kampuni hiyo.

Washtakiwa ni Herington Sakaya (29), mhasibu na mkazi wa Kigamboni; Buheri Komba (36), ofisa mauzo na mkazi wa Temeke; Hemed Ramadhani (33)ofisa mauzo na mkazi wa Sabasaba Mbagala; Bilal Mtemelo (28) ofisa masoko na mkazi wa Mtoni kwa Aziz ally na Said Bakari (32) ofisa masoko na mkazi wa Kigamboni.

Wengine  ni ofisa mauzo, Simon Magee (37) mkazi wa Mbagala na Nusra Kibuda (26) mkazi wa Kijichi; Salome Sanga (35) mhasibu na mkazi wa Igawilo mkoani Mbeya na Said Hamis Said (27) ofisa mauzo na mkazi wa Kigamboni.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo jana jioni, Januari 16, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 957 ya mwaka 2026 yenye mashtaka tisa yakiwemo ya wizi na kutakatisha fedha.

Hata hivyo, mshtakiwa Sanga na Said hawakuwepo mahakamani hapo, hivyo watasomewa mashtaka yao watakapofikishwa mahakamani hapo.

Kabla ya kuwasomea mashtaka yao, hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga aliwaeleza washtakiwa hao kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya namna ya namna hiyo labda kwa kibali maalumu.

Washtakiwa ambao ni wafanyakazi wa Kampuni ya Vita foam (T) Limited, wakiwa chini ya ulinzi wa polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya uhujumu uchumi. Picha na Hadija Jumanne



Pia washtakiwa hawatadhaminika kwa kuwa mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kutoa ufafanuzi huo, washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali Tumaini Mafuru.

Mafuru alidai shtaka la kwanza ni la wizi wakiwa wafanyakazi wa kampuni ya Vita Foam (T) Limited linalomkabili Sakaya, Ramadhani, Magee, Kibuda na Saidi.

Alidai washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 1, 2023 na Oktoba 31, 2024 katika jiji la Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa kampuni ya kampuni ya Vita Foam (T) Limited, wanadaiwa kuiba Sh324milioni, mali ya mwajiri wao.

Shtaka pili ni kutakatisha fedha, linalomkabili Sakaya, Ramadhani, Magee, Kibuda na Saidi, ambapo siku na eneo hilo, washtakiwa walijipatia fedha hizo wakati wakijua, fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la wizi.

Shtaka la tatu ni la wizi na linamkabili mshtakiwa Sayaka, Bakari, Magee, Kibuda na Said, ambapo katika kipindi hicho siku na eneo hilo, wanadaiwa kuiba Sh321.6milioni mali ya mwajiri wao na shtaka la nne washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Mafuru alidai shtaka la tano ni la wizi na linamkabili Sakaya, Mtemelo, Magee, Kibuda na Saidi, ambapo siku na eneo hilo, waliiba Sh241.5milioni mali ya mwajiri wao, huku shtaka la sita ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha linalokabili washtakiwa hao watano.

Shtaka la saba ni la wizi na linawakabili Sakaya, Komba, Magee, Kibuda na Said, ambapo katika kipindi hicho, wanadaiwa kuiba Sh557.9milioni mali ya mwajiri wao na pia wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha, wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi.

Mahakama iliendelea kuelezwa kuwa shtaka la tisa ni la wizi  linamkabili Sakaya, Magee, Kibuda, Sanga na Said, ambapo katika kipindi hicho ndani ya jiji la Dar es salaam, wanadaiwa kuiba Sh32.7milioni mali ya mwajiri wao.

Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi haujakamilika na kwamba wanaomba mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mwankuga aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 29, 2026 kwa kutajwa na washtakiwa wamepelekwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana.