Unguja. Wakati maonyesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar (ZITF) yakifungwa, Wafanyabiashara wamesisitiza ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma na kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara ili wajasiriamali na wafanyabiashara waweze kukua na kushindana kikanda na kimataifa.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Zanzibar (ZMCC), Ali Amour amesema hatua hiyo itachangia zaidi katika kuongeza ajira na kukuza vipato nchini.
“Tunasisitiza ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma, na kuimarisha mazingira ya kufanya biashara hatua itakayokuza biashara nchini na kuongeza ajira,” amesema Amour wakati wa kufunga maonesho hayo Januari 17, 2026, Unguja Zanzibar
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo, amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu ya kukutanisha wafanyabiashara kutoka ndani na nje, yamefungua milango na fursa mpya za biashara, ushirikiano na masoko.
“Yamewezesha wajasiriamali kuonyesha bidhaa zao na kujifunza kutoka kwa wenzao na kujijengea mtandao wa kibiashara yenye tija,” amesema
Kupitia biashara ya viwanda, kilimo ubunifu na ujasiriamali, Amour amesema nchi inaendelea kujenga uchumi jumuishi unaonufaisha wananchi wengi zaidi.
“Tunawataka wafanyabiashara kutumia fursa ya maonesho haya kama mwanzo wa safari mpya ya kibiashara, kuendeleza mawasiliano, mikataba na ushirikiano kwani maonesho haya iwe chachu ya maendeleo endelevu ya biashara,” amesema
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dk Habiba Hassan Omar amesema katika maonesho hayo yamejumuisha washiriki 316 kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na nje ya nchi.
Amesema lengo kubwa la tamasha hilo ni kuwakutanisha wafanyabiashara na wajasiriamali kubadilishana mawazo, ujuzi wa ubunifu na kupata masoko ya biashara zao.
“Maonyesho ya mwaka huu pamoja na kuwapo wafanyabiashara, kuna taasisi mbalimbali za serikali kuonesha huduma zinazotolewa katika siku za kila siku,” amesema.
Katika kipindi chote cha maonesho kwa takribani siku 19, katika eneo hilo kulikuwa na mijadala mbalimbali kuhusiana na masuala ya uwekezaji, fedha, ubunifu na ilikuwepo siku ya mswahili ambayo ilihusisha burudani mbalimbali.
Dk Habiba amesema changamoto ni moja ya njia kuleta ufanisi, “ili ufanikiwe lazima uzipate, kwa hiyo lolote ambalo limekwaza katika eneo hili na kwa sababu tupo wengi tupo tayari kuzipokea ili turekebishe katika mwaka ujao zisijirejee tena,” amesema
Akifunga maonesho hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema maonesho hayo ni mwendelezo wa yaliyopita.
Amesema katika maonesho mbali na kutoa fursa kwa washiriki lakini husaidia wananchi kujipatia bidhaa na huduma mbalimbali kwa gharama nafuu.
“Maonesho ni fursa pekee ya kuwakutanisha watu mbalimbali, wafanyabiashara, wazalishaji na watumiaji wa bidhaa mbalimbali, serikali itaendelea kuweka mkazo kuhakikisha yanaboreshwa maonesho hayo ili yaendelee kuleta tija kubwa zaidi.
Kwa mara ya kwanza maonesho hayo yalizinduliwa katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo liliitwa tamasha la biashara Zanzibar, serikali iliamua yawe endelevu kwa ajili ya kukuza biashara na kisiwani humo.