Dar es Salaam. Kauli ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ya kutaka usimamizi wa mitihani ya vyuo na kada za afya kuhamishiwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imeibua mjadala miongoni mwa wadau wa sekta ya afya.
Wapo wanaounga mkono hoja hiyo kwa misingi ya kisera, na wengine wakionya kuhusu hatari ya kushusha viwango vya wataalamu wa afya iwapo mabadiliko hayo hayataandaliwa kwa kina.
Akizungumza Januari 14, 2026, wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, Waziri Mchengerwa alisema wizara hiyo inatumia karibu Sh20 bilioni kusimamia mitihani ya kada za afya, gharama alizosema hazina tija ikilinganishwa na majukumu ya msingi ya wizara.
“Afya nasikia karibu bilioni 20 inatumika kusimamia mitihani. Wizara ya Elimu ipo, majukumu hayo yaende Wizara ya Elimu, fedha zibaki hapa zifanye kazi nyingine za msingi,” alisema huku akisisitiza kuwa katika kipindi chake hali hiyo haitaendelea.
Kauli hiyo imeungwa mkono kwa tahadhari na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, alipozungumza na Mwananchi jana, Januari 17, 2026, akisema hatua hiyo inapaswa kuangaliwa katika muktadha wa kihistoria na mabadiliko ya mifumo ya elimu nchini.
Amesema baada ya Uhuru, sekta nyingi, zikiwamo za afya, maji na nyingine, zililazimika kuanzisha mifumo ya mafunzo nje ya Wizara ya Elimu kutokana na uhaba wa wataalamu.
Hata hivyo, Dk Nkoronko amesema mazingira yamebadilika na sasa kuna haja ya kufanya tathmini ya kina kama mifumo ya sasa bado inahitajika.
“Ni agizo la kisera, linahitaji tathmini ya mifumo yetu ya elimu, kama inaweza kusimamia kirahisi mafunzo na mitihani ya kada za afya bila kuathiri ubora,” amesema, akiongeza kuwa gharama za mitihani zinapaswa pia kuangaliwa upya, ikiwemo matumizi ya Tehama ili kuendana na teknolojia na kupunguza gharama.
Kwa upande mwingine, Dk Ezekiel Mbao, ambaye ni Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), amesema Wizara ya Afya ni nyeti, inayohusika moja kwa moja na uhai wa binadamu, hivyo usimamizi wa mitihani ya wataalamu wake haupaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa kawaida wa elimu.
“Kwa lugha rahisi, unaweza kusema ni mitihani tu, lakini kwa mtaalamu wa afya, ni mitihani ya kipekee inayohitaji kusimamiwa na watu wanaoelewa mahitaji ya jamii na viwango vya taaluma,” amesema daktari huyo.
Ameonya kuwa kuhamishia jukumu hilo Wizara ya Elimu bila kuijengea uwezo wa kitaalamu kunaweza kusababisha kuzalishwa kwa wataalamu wasio na viwango, hasa katika kipindi ambacho kuna wimbi kubwa la uanzishwaji wa vyuo vya afya.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Tanzania (APHFTA), Dk Samwel Ogillo, amesema hoja ya Waziri Mchengerwa ina mantiki ya kisera kwa kuwa Wizara ya Elimu ndiyo yenye dhamana ya kusimamia mitihani ya sekta zote nchini.
Amefafanua kwamba kuhamishwa kwa usimamizi hakumaanishi wataalamu wa afya wataondolewa katika mchakato wa tathmini, bali msimamizi mkuu atakuwa Wizara ya Elimu huku wataalamu wa afya wakiendelea kufanya kazi za kitaalamu.
“Sekta binafsi inamiliki zaidi ya asilimia 50 ya vyuo vya afya, hivyo nayo inapaswa kuhusishwa. Tumpe waziri nafasi ya kutekeleza, kisha tuone tofauti itakuwaje,” amesema.
Kwa ujumla, wadau wameeleza kuwa agizo hilo linafungua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa elimu ya kati ya kada za afya nchini, huku wengi wakisisitiza umuhimu wa maandalizi ya kina, ushirikishwaji wa wadau na ulinzi wa viwango vya taaluma kabla ya utekelezaji wake.
Katika maagizo yake, mbali na suala la mitihani, Waziri Mchengerwa pia aliielekeza Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara ya Elimu kuvipa hadhi vyuo vya afya vya Serikali, akisema kushuka kwa ubora kumesababisha wanafunzi wengi kukimbilia vyuo binafsi.
“Muende mkajipange vizuri ili vyuo vya Serikali vizalishe ‘cream’,” alisema.