Auawa akidaiwa kutembea na mke wa mtu

Tabora. Kijana mmoja anayefahamika kwa jina la Joseph Madaha, mkazi wa Kitongoji cha Kipela Magharibi, Kata ya Tumbi, Manispaa ya Tabora, amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa  kupigwa na kisha kukatwa sikio, akidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa mtu.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumapili Januari 18, 2026, Mwenyekiti wa Kijiji cha Tumbi, Manispaa ya Tabora, Rajabu Hamsini amesema alipigiwa simu na mwananchi wa kijiji hicho saa sita usiku, akitaarifiwa kuwa watu wasiojulikana wamemvamia Joseph na kumjeruhi kisha kutokomea kusikojulikana.

Amesema kutokana na kuwa ilikuwa usiku wa manane, walikubaliana waanze kumtafuta kukipambazuka.

Amesema kabla ya kuelekea maeneo mengine asubuhi, walianzia kwenye chumba alichokuwa akiishi, huko walikutana na kipande cha sikio, godoro lililochanwa pamoja na damu nyingi chini, hali iliyoashiria tukio la vurugu.

Ameongeza kuwa baada ya kufuatilia taarifa zaidi, mwili wa marehemu ulipatikana katika eneo la shamba lililopo jirani na nyumba aliyokuwa akiishi.

“Tumeambiwa na shemeji yake kwamba walifika watu wanne ambao hawakuwafahamu, wakasema wanamtafuta Joseph ndipo wakaanza kumpiga wakidai amechukua mke wa mtu,” amesema Hamsini.

Nyumba aliyokua anaishi Joseph Madaha enzi za uhai akilima mashamba kama sehemu ya ajira yake.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kipela Magharibi, Maganga Kwabi amesema washambuliaji walidai kuwa Joseph alikuwa na uhusiano na mke wa mtu na kwamba, alikuwa amemnunulia simu, hivyo walitaka apigwe na akatwe sikio ili iwe alama ya onyo, wakidai kuwa hawakuwa na nia ya kumuua.

“Hawakusema kuwa wanataka kumuua, bali walidai wanataka apate alama na aache tabia ya kuchukua wake za watu, lakini walimpiga kiasi cha kusababisha majeraha makubwa yaliyompelekea kupoteza maisha,” amedai.

Naye James Madaha, kaka wa marehemu, amesema alipewa taarifa na mtu aliyekuwa karibu na Joseph kuwa amepigwa saa moja usiku.

Amesema aliamua kwenda nyumbani kwake, lakini hakumkuta, ndipo juhudi za kumtafuta zilipoanza hadi mwili wake ulipopatikana shambani. Amesema marehemu alikuwa na familia yake inayoishi mkoani Kigoma.

“Wanasema amepigwa kwa madai ya kuchukua mke wa mtu hapa Tumbi, lakini mimi sifahamu hilo. Labda kama aliamua kunificha, lakini adhabu zipo nyingi, kwa nini wafikie hatua ya kuniulia ndugu yangu,” amesema James akibubujikwa machozi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi amekiri kutokea kwa tukio hilo na amewaonya wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Kamanda Mbogani amesisitiza kuwa kila mtu bila kujali tuhuma zinazomkabili, ana haki ya kuishi kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa kijiji cha Tumbi manispaa ya Tabora Rajabu Hamsini akizungumzia tukio la mauaji kijijini hapo.



Amesema wivu wa mapenzi unatajwa kuwa chanzo cha tukio hilo, marehemu anadaiwa kuwa na uhusiano na mke wa mtu hadi kufikia hatua ya kumnunulia simu, huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi ili kubaini undani wa tukio hilo.

“Tupo kazini na tutaendelea kuwatafuta na kuwakamata wote waliohusika na tukio hili, kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria,” amesema Kamanda Mbogambi.