Arusha. Mahakama ya Rufaa nchini imebariki uamuzi wa Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza Kuu la Rufaa za Kodi (TRAT), ya kukataa maombi ya Bank of Africa Tanzania Limited, zilizoruhusu kutozwa kodi zaidi ya Sh240.5 milioni.
Katika uamuzi wake, TRAB, iliweka kodi ya mshahara (Pay As You Earn – PAYE) kwenye mafao yanayotozwa kodi yaliyolipwa kwa wafanyakazi wawili wa kigeni wa mrufani.
Pili, ilijumuisha mchango wa Bima ya Maisha ya Kikundi katika uamuzi wa mapato yanayotozwa kodi ya wafanyakazi hao kwa mwaka wa kodi 2019.
Aidha, ilijumuisha ada za shule zilizolipwa na mrufani katika hesabu ya mapato yanayotozwa kodi ya wafanyakazi hao kwa mwaka wa kodi 2019.
Kati ya fedha hizo Sh 225.6 milioni zilikuwa kodi kuu huku zaidi ya Sh14.9milioni zikiwa ni riba.
Benki hiyo ilikata rufaa dhidi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hukumu hiyo imetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao ni Shaaban Lila, Penterine Kente na Abraham Mwampashi waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo ya madai namba 166/2025.
Jopo hilo baada ya kupitia mwenendo na kusikiliza hoja za pande zote ilikubaliana kuwa malipo ya bima ya maisha ya kikundi na ada za shule zilizolipwa na benki hiyo kwa niaba ya wafanyakazi wake ni faida zinazotokana na ajira hivyo zinapaswa kujumuishwa katika mapato yanayotozwa kodi kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004.
Mahakama hiyo baada ya kuchambua hoja zote Mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo kwa gharama baada ya kutupilia mbali sababu zote nne za rufaa kutokana na kutokuwa na mashiko kisheria.
Aidha ilieleza wanakubaliana kuwa kutoza riba pale ambapo mlipa kodi anashindwa kulipa kodi iliyowekwa ni matokeo yasiyoepukika ambapo mlipakodi anawajibika kulipa mapka na kodi.
Rufaa hiyo ilitokana na ukaguzi wa kodi uliofanywa na TRA mwaka 2020 kwa mwaka wa mapato 2019 kuhusiana na masuala la kodi ya mrufani, ambapo Mamlaka hiyo Desemba 11, 2020 alitoa cheti cha Paye akidai kwa mrufani zaidi ya Sh225.6 milioni kama kodi kuu na zaidi ya Sh14.906 milioni kama riba yake.
Januari 2021, benki hiyo ilipinga cheti hicho kwa misingi miwili akidai kuwa TRA ilikokotoa vibaya Paye kwenye mpango wa faida za kodi aliokuwa nao na wafanyakazi wake wawili wa kigeni.
Sababu nyingine ni kwamba ilijumuisha isivyostahili gharama za bima ya maisha ya kikundi pamoja na ada za shule katika mapato yanayotoza kodi ya wafanyakazi.
Mjibu rufaa alishikilia msimamo wake kwamba Paye ya marupurupu ya kodi iliwekwa kwa mujibu wa kifungu cha 27 (1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004.
Hata hivyo, pingamizi hilo lilitupiliwa mbali hatua iliyosababisha benki kukata rufaa TRAB, na baadaye TRAT,ambazo zote mbili ziliunga mkono uamuzi wa TRA.
Rufaa ya sasa
Katika rufaa hiyo, benki hiyo inapinga uamuzi wa baraza ikiwa na sababu nne ambazo ni baraza hilo lilifanya makosa kisheria kwa kushidwa kuchanganua ushahidi ulioandikwa vibaya na kwa kutafsiri vibaya vifungu vya 27(1) (d) kikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 18 (2) (b) cha Sheria ya Ushuru wa Mapato.
Nyingine ni baraza hilo lilifanya makosa kisheria katika tafsiri yake ya kifungu cha 7(2) (b) cha Sheria tajwa juu kwa kuhitimisha kwamba malipo yanayolipwa na mrufani chini ya bima ya maisha ya kikundi ni sehemu ya viambatisho katika kuhesabu faida au faida ya wafanyakazi kutokana na ajira.
Sababu nyingine ni baraza hilo lilifanya makosa kisheria kwa kushindwa kutathmini ushahidi ulioandikwa na kutafsiriwa vibaya masharti ya kifungu cha 7 (2) (c) cha Sheria ya Ushuru wa Mapato katika kuhitimisha kwamba ada za shule zinazolipwa na mrufani kwa wafanyakazi wake ni faida kwa wafanyakazi.
Sababu ya nne ilikuwa Baraza lilifanya makosa kwa kuhitimisha kwamba kutoza riba kwa malipo ya kuchelewa chini ya kifungu cha 76 cha Sheria ya Utawa wa Ushuru na dhabu ilikuwa halali.
Kwa upande wake, mjibu rufaa alitetea uamuzi wa TRAB na TRAT ikisisitiza kuwa hoja nyingi za benki zilihitaji Mahakama kupitia upya ushahidi, jambo ambalo liko nje ya mamlaka yake na kuwa malipo ya bima ya maisha ya kikundi yalikuwa wajibu wa wafanyakazi, hivyo malipo yaliyofanywa na benki kwa niaba yao yaliwapatia faida ya moja kwa moja.
Walieleza kuwa suala hilo liliangukia chini ya kifungu cha 7(2) (b) cha Sheria ya Kodi ya Mapato,huku kuhusu ada za shule, ilielezwa kuwa nazo ni faida inayotokana na ajira na hivyo kutozwa kodi ni sahihi.
Uamuzi wa Mahakama
Baada ya kupitia mwenendo na kusikiliza hoja za pande zote mbili, Majaji hao walieleza kuwa baadhi ya sababu za rufaa, hususan zinazohusu madai ya kutotathminiwa kwa ushahidi ipasavyo, zilikiuka kifungu cha 25(2) cha Sheria ya Rufaa za Ushuru kwa kuwa zilichanganya masuala ya sheria na ukweli.
Mahakama ilisema haina mamlaka ya kuingia kwenye tathmini upya ya ushahidi uliotolewa mbele ya TRAT.
Kuhusu bima ya maisha ya kikundi, Mahakama ilibainisha kuwa malipo hayo yalimuondolea mfanyakazi wajibu wa kulipa bima yake binafsi, hivyo yalikuwa faida inayotokana na ajira na kuwa bima ya maisha ni tofauti na bima ya matibabu, na hivyo haiwezi kufaidika na msamaha wa kodi.
Majaji hao walikataa hoja kuwa malipo hayo hayangeweza kugawanywa kwa wafanyakazi binafsi, ikisema kuwa kiasi kilicholipwa na idadi ya wafanyakazi waliostahiki vilijulikana, hivyo haikuwa vigumu kiutawala kufanya mgawanyo huo.
Kuhusu riba na adhabu, Mahakama ilisisitiza kuwa chini ya kifungu cha 76 (1) cha Sheria ya Utawala wa Ushuru ya mwaka 2015, kutoza riba ni sharti la kisheria pale mlipakodi anaposhindwa kulipa kodi kwa wakati.
“Kutoza riba pale mlipakodi anashindwa kulipa kodi iliyowekwa ni matokeo yasiyoepukika ambayo mlipakodi anawajibika kulipa.Kwa sababu zilizotajwa juu tunaona rufaa haina msingi na kuitupilia mbali kwa gharama,”amehitimisha Jaji Mwampashi.