Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk Vicent Anney ametoa wito kwa walimu wakuu, walimu wa taaluma pamoja na wazazi na walezi kushirikiana kwa karibu ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi, hususan wanafunzi wa madarasa ya mitihani likiwamo la nne na la saba.
Akizungumza Januari 18, 2025 wakati wa kikao cha tathmini ya elimu wilayani humo amesema kuwa hakuna sababu ya ufaulu kuendelea kuwa wa chini ilhali Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa madarasa, upatikanaji wa walimu na vifaa vya kufundishia.
Amesema matumizi ya vipindi vya ziada, ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi mmojammoja pamoja na kupambana na utoro wa wanafunzi ni miongoni mwa mambo yanayosaidia kuongeza ufaulu.
“Ufaulu ni matokeo ya mshikamano. Walimu wafanye kazi kwa bidii, wazazi wahakikishe watoto wanahudhuria shule kila siku, na wanafunzi wajitume kusoma,” amesema.
Pia amesisitiza kuwa wanafunzi wote walioandikishwa darasa la awali na darasa la kwanza kuanza masomo mara moja kwani wilaya hiyo imejipanga kupambana na utoro.
Dk Anney ametumia fursa hiyo kuwaonya wazazi wanaowatumia watoto katika shughuli zisizo za kielimu wakati wa masomo akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu ya Awali na Msingi wilayani humo, Godfrey Kalulu, akiwasilisha taarifa ya matokeo ya mitihani ya kitaifa kwa mwaka 2025, amesema wilaya hiyo imeendelea kupiga hatua kielimu.
Amesema ufaulu wa darasa la saba umefikia asilimia 79.02 mwaka 2025, ukilinganishwa na asilimia 75.75 mwaka 2024, huku ufaulu wa darasa la nne ukipanda hadi asilimia 85.74, kutoka asilimia 76.8 mwaka 2024, hatua iliyoiwezesha wilaya kuvuka lengo la kitaifa la ufaulu la asilimia 80.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano baina ya walimu, uongozi wa shule, wazazi na Serikali, huku akiwapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka kuongeza juhudi zaidi ili matokeo yaendelee kuimarika.
“Ndiyo maana leo tumekutana hapa kwa pamoja kufanya tathimini na kupongezana kwa yote tuliyoyafanya mazuri katika kuongeza ufaulu kiwilaya katika mitihani ya darasa la saba na darasa la nne, jambo la msingi kila mmoja wetu atimize wajibu wake,”amesema.
Amesema kuwa hatua hizi zinalenga kuhakikisha wilaya inaendelea kupandisha viwango vya ufaulu na ushindani wa kitaaluma, sambamba na dira ya Serikali ya kuboresha elimu ya msingi nchini.
Nazahedi Mweteni ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kulimi, amesema mafanikio hayo yametokana na nidhamu na ufuatiliaji wa karibu wa wanafunzi.
“Tumeimarisha vipindi vya ziada, tathmini za mara kwa mara na ushirikiano mzuri na wazazi. Matokeo haya yanatupa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, Devotha Soko ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kidema, amesema kuongezeka kwa ufaulu ni ishara kuwa walimu wameanza kuona matunda ya juhudi zao licha ya changamoto zilizopo.
“Changamoto zipo, lakini moyo wa kujitolea kwa walimu umechangia sana. Tunapoona matokeo yanapanda, hata morali ya kufundisha inaongezeka,” amesema.
Naye Frola Joseph, mwalimu wa Shule ya Msingi Sola, amesisitiza umuhimu wa motisha kwa walimu na mazingira rafiki ya kufundishia.
“Tunapopata ushirikiano kutoka kwa viongozi na wazazi, kazi yetu inakuwa rahisi. Tunaamini tukiongezewa motisha na vifaa, ufaulu unaweza kupanda zaidi ya hapa,” amesema.