Hussein Masalanga atua Yanga | Mwanaspoti

KLABU ya Yanga, imemchukua kwa mkopo wa miezi sita golikipa wa Singida Black Stars, Hussein Masalanga ambaye atahudumu kikosini hapo hadi mwisho wa msimu huu.

Uamuzi wa Yanga kumchukua Msalanga umetokana na kipa wake, Khomein Abubakar kupata majeraha ambayo yatamuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, Masalanga usajili wake ni wa dharura na atadumu kikosini hapo kwa miezi sita.

“Ni kweli Masalanga ametua Yanga kwa mkopo wa miezi sita akichukua nafasi ya Khomein aliyeumia ambapo jeraha lake si la kupona haraka, ndio maana umefanyika usajili huo,” kimesema chanzo hicho.

Chanzo kimeendelea kubainisha kuwa, Khomein kwa sasa anaondolewa katika orodha ya majina ya wachezaji wa Yanga ili kumuachia nafasi Masalanga.

Hata hivyo, kipa huyo ambaye mkataba wake na Yanga unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu, ataendelea kutibiwa klabu hapo na kutambulika kama mchezaji wa kikosi hicho hadi atakapopona.

Ikumbukwe Masalanga hivi karibuni alikuwa na kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika michuano ya AFCON 2025 na kudaka mechi mbili dhidi ya Tunisia hatua ya makundi na Morocco hatua ya 16 Bora.

Usajili huo wa Masalanga anayechukua nafasi ya Khomein, unafanya Yanga kuendelea kuwa na makipa watatu ambao ni Djigui Diarra na Aboutwalib Mshery.

Huyu ni mchezaji wa tano mpya katika usajili huu wa dirisha dogo kutua Yanga baada ya Emmanuel Mwanengo, Mohamed Damaro, Allan Okello na Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’.