Jeshi lakosolewa kuingilia uchaguzi Uganda, Bobi Wine agomea matokeo

Kampala, Uganda. Waangalizi wa uchaguzi wamelikosoa vikali Jeshi la Uganda (UPDF) kwa kutoa maelekezo yanayohusu mwenendo wa uchaguzi, wakisema hatua hiyo inakiuka misingi ya uhuru na uwazi wa mchakato wa kidemokrasia.

Katika taarifa ya NTV Uganda, wachunguzi hao wamesema walishtushwa na tamko la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, aliyewaagiza wapigakura kuondoka na kutojirundika katika vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura zao.

Kwa mujibu wa wachunguzi hao, kauli hiyo ilizua hofu na maswali kuhusu nafasi ya jeshi katika usimamizi wa uchaguzi, huku wakisisitiza kuwa masuala ya uchaguzi yanapaswa kusimamiwa kikamilifu na Tume ya Uchaguzi, bila kuingiliwa na vyombo vya ulinzi.

Hayo yanajiri wakati matokeo yakitangazwa ambapo Yoweri Museveni ameshinda kiti cha urais kwa muhula wa saba kwa asilimia 71.6 huku mpinzani wake Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine akipata asilimia 24.7.

Ujumbe wa waangalizi hao, ulioongozwa na Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan, umependekeza uchaguzi ubaki nje ya mamlaka ya jeshi, na  maofisa wa kijeshi wajiepushe kutoa kauli au maelekezo ambayo kikatiba na kisheria yanapaswa kutolewa na Tume ya Uchaguzi.

Wamesema ushiriki au kauli za jeshi katika masuala ya uchaguzi zinaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa mchakato wa uchaguzi na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

Katika hatua nyingine Bobi Wine ambaye amegombea urais kupitia chama cha National Unity Platform (NUP), ameyapinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi, ambayo yamemtangaza Rais aliyepo madarakani, Yoweri Museveni, kuwa mshindi.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, ushindi wa Rais Museveni unamwezesha kuendelea kubaki madarakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano, hatua inayomfanya aendelee kuorodheshwa miongoni mwa viongozi wa Afrika waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi.

Iwapo atamaliza muhula huu, Rais Museveni atakuwa ameiongoza Uganda kwa jumla ya miaka 45, tangu alipoingia madarakani mwaka 1986.

Hata hivyo, Bobi Wine amesema hatambui matokeo hayo, akidai kulikuwa na dosari katika mchakato wa uchaguzi, ingawa hakutoa maelezo ya kina kuhusu hatua atakazochukua kufuatia msimamo wake huo.

Rais Museveni anatarajiwa kuapishwa rasmi kuanza muhula wake mpya katika itakayotolewa na wahusika.