VIONGOZI wa Mendiola inayoshiriki Ligi Kuu Ufilipino wako kwenye mchakato wa kumboreshea mkataba winga wa Kitanzania, John Mgong’os baada ya kuridhishwa na kiwango chake.
Mgong’os alijiunga na timu hiyo akitokea Hua Hin iliyokuwa inashiriki Ligi daraja la pili Thailand na aliitumikia msimu mmoja akifunga mabao manane.
Taarifa mbalimbali kutoka Ufilipino zinaeleza Mendiola imeridhishwa na kiwango cha winga huyo na sasa iko tayari kukaa mezani kuzungumza juu ya kumboreshea mkataba.
Vyombo mbalimbali vimeripoti timu mbalimbali kwenye ligi hiyo vinaulizia uwezekano wa kumpata Mgong’os hivyo inahakikisha kumshawishi ili aweze kusalia.
“Huenda akasalia kwa sababu timu hiyo imeweka ofa nzuri mkataba wake unatamatika mwishoni mwa msimu huu kuna timu zimepeleka ofa nzuri kwa timu wakihitaji saini yake.” ilisema moja ya taarifa hiyo.
Winga huyo alisaini mkataba wa mwaka mmoja Septemba mwaka jana uliokuwa na kipengele cha kuongeza mingine kama ataonyesha kiwango kizuri, kwenye mechi tisa amecheza dakika 144 bila bao.