Kihongosi asisitiza umoja, mshikamano na upendo

Manyoni. Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kenan Kihongosi amewataka viongozi na wananchi kufanya kazi kwa umoja, mshikamano na upendo.

Kihongosi ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 18,2026 wakati wa mapokezi katika ofisi ya CCM Wilaya ya Manyoni ambayo ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano katika Mkoa wa Singida.

Ziara hiyo inalenga kuhakikisha chama kinawafikia wanachama wote nchini sambamba na kusikiliza kero za wananchi, na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Akiwa katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Manyoni, kiongozi huyo amezungumza na wananchi waliofurika kumpokea kabla ya kwenda kuzungumza na wananchi.

Picha za Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo Kenan Kihongosi katika picha tofauti tofauti alipoingia Mkoa wa Singida.



“Lazima tufanye kazi kwa umoja, mshikamano na upendo lakini tuwatumikie wananchi wetu wakati wote,” amesisitiza Kihongosi.
Akizungumza na wanachama na wananchi kwenye mkutano wa Shina namba 7 wilayani Manyoni, amewataka viongozi kushirikiana na kuwatumikia wananchi.

Kwa mujibu wa Kihongosi, ushirikiano ndiyo siri ya ushindi wa CCM ambao wengi wamekuwa wakihoji bila kujua msingi wa chama hicho kikongwe unaanzia ngazi ya chini.

Amesema hakuna anayeweza kusimulia mambo mazuri bila kutaja CCM ambacho nacho kimekuwa na siri ya ushindi kwa sababu ya mshikamano.

Kiongozi huyo amewataka vijana kulinda nchi yao kwa namna yoyote na waachane na udanganyifu kutoka kwa wanaotaka kuichoma nchi kwa sababu ya kudanganywa.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata amesema wakati wote wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na ndiyo siri ya kuwafanya wawe kitu kimoja.

Mlata amesema matatizo mengi yamepungua katika mkoa huo kwa sababu ya utulivu mkubwa uliotokana na Umoja walionao.