KIHONGOSI ATEMBELEA NA KUKAGUA UJENZI NA UKARABATI WA HOSPITALI YA WILAYA YA MANYONI

Katibu wa NEC Itikadi uenezi na mafunzo CCM, Ndugu Kenani Labani Kihongosi, ametembelea na kukagua ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, mradi uliokamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.4.

Hospitali hiyo ina majengo yote muhimu pamoja na vifaa vya kisasa vya tiba, vinavyoboresh­a huduma za afya kwa wananchi wa Manyoni na maeneo ya jirani, hususan katika kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuongeza ufanisi wa huduma za afya.

Akizungumza baada ya ukaguzi, Ndugu Kihongosi alitoa pongezi za dhati kwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuelekeza fedha nyingi katika sekta ya afya, akisisitiza kuwa huo ni ushahidi wa uongozi unaoweka mbele maslahi ya wananchi.

Aidha, aliwapongeza wananchi wa Manyoni kwa ushiriki wao katika shughuli za maendeleo, akieleza kuwa mchango wa wananchi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa. Vilevile aliipongeza Serikali kwa usimamizi mzuri na uwajibikaji wa mradi huo uliogharimu fedha nyingi za umma.

Ndugu Kihongosi aliwataka Watanzania kutembea na kujionea kwa vitendo kasi ya maendeleo inayopatikana chini ya Serikali ya CCM, akisisitiza kuwa CCM ni Chama cha vitendo, matokeo na maendeleo ya kweli.